Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

07- Abu Ruqayyah Tamiym bin Aws ad-Daariy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Dini ni nasaha.” Tukauliza: “Kwa nani?” Akasema kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, kwa Viongozi wa Waislamu na watu wa kawaida.”

MAELEZO

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… Kitabu Chake…”

Bi maana nasaha inayostahiki Kitabu ambayo ni Qur-aan. Ikiwa na maana ya kwamba mtu aipe Qur-aan haki yake. Huko ni kwa kuamini kuwa ni maneno ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) Aliyotamka kwayo. Ni ishara kubwa. Qur-aan ndio ishara kubwa waliyopewa Mitume. Qur-aan ndio hoja kubwa mpaka Qiyaamah kitaposimama. Ndani ya Qur-aan mna uongofu na nuru. Allaah (Ta´ala) Amesema:

إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ

“Hakika hii Qur-aan inaongoza katika yaliyonyooka kabisa.” (17:09)

Ni wajibu kujisalimisha kwa yale Aliyoamrisha Allaah. Ni wajibu kujiepusha na yale Aliyokataza. Ni wajibu kusadikisha yale Aliyoelezea bila ya kuwa na mashaka na mengineyo katika mambo ambayo Qur-aan inastahiki.

Miongoni vilevile mwa nasaha zinazopendekezwa kwa Qur-aan ni mtu kuisoma kwa wingi na asiisuse katika kuisoma, kuizingatia, kujitibu kwayo na mfano wa hayo katika mambo yaliyokuja katika Sunnah katika haki ya Qur-aan.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Arba´iyn an-Nawawiyyah, uk. 161
  • Imechapishwa: 17/05/2020