Swali: Ni ushauri gani ambao baba yetu Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz anampa ambaye hatoi zakaah? Ushauri ambao huenda ukalainisha moyo wake na kumrudisha katika usawa.

Jibu: Kama angelikuwa amesikia huko nyuma – ikiwa alikuwa karibu – basi angepata cha kutosha cha kuutikisa moyo wake ili atimize kile ambacho Allaah amemlazimisha katika zakaah. Nasaha zangu kwa kila anayebakhili kwa zakaah amche Allaah na akumbuke kuwa Yule aliyempa mali ndiye aliyemjaribu kwa hiyo mali. Aliyemruzuku hiyo mali ndiye aliyempa mtihani. Akiishukuru neema hiyo na akatoa haki yake, basi amefaulu. Lakini akibakhili kwa zakaah na asipotoa haki ya neema hiyo, basi amepata khasara na ameshindwa na ataonja adhabu yake; adhabu ya kaburini na adhabu ya siku ya Qiyaamah. Tunamwomba Allaah atujaalie salama. Mali ni yenye kuondoka na jambo lake ni jepesi, lakini matokeo yake ni mabaya mno kwa yule anayebakhili kwa haki yake na asiyetoa wajibu wake. Unakusanya mali kutoka kila njia, kisha unaiacha kwa wale watakaokuja baada yako, huku hesabu yake na madhara yake yanabaki juu yako. Basi amche Allaah na ukumbuke kusimama mbele Yake na kwamba atamlipa kila mtenda kwa matendo yake. Aidha ujue kuwa mali ni mtihani, kama alivyosema Allaah (Ta´ala):

إِنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ

”Hakika si venginevyo mali zenu na watoto wenu ni jaribio.”[1]

وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً

“Tutakujaribuni kwa mitihani ya shari na kheri.”[2]

Kwa hiyo mali ni jaribio na mtihani. Ukiishukuru neema hiyo, ukatoa haki yake na ukaielekeza katika matumizi ya halali, umepata mafanikio makubwa na mali hiyo inakuwa neema iliyo bora kwako. Hakika mali ni mwenza mzuri kwa muumini: anaunga nayo undugu wa damu, analipa haki anazowajibika, anashiriki katika miradi ya kheri, anawasaidia wanyonge na kuwafariji. Hivyo mali inakuwa neema kubwa kwake. Lakini akiibakhili na asitoe haki yake, basi inakuwa balaa kubwa kwake na malipo yake yatakuwa mabaya.

[1] 64:15

[2]21:35

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1078/نصيحة-لمن-لا-يودي-الزكاة
  • Imechapishwa: 17/02/2026