21. Baadhi ya hukumu kuhusu kulipa deni la Ramadhaan

Mlango wa nne: Kulipa, swawm iliyopendekezwa, yaliyochukizwa na kuharamishwa wakati wa kufunga. Ndani yake kuna masuala yafuatayo:

Suala la kwanza: Kulipa funga

Mtu akila siku miongoni mwa siku za Ramadhaan basi ni lazima kwake kutubu kwa Allaah na amwombe msamaha. Kwa sababu hiyo ni jarima na dhambi kubwa. Pamoja na kutubu na kuomba msamaha ni lazima pia kulipa kiasi cha siku alizokula baada ya Ramadhaan.

Ulazima wa kulipa katika hali hii ni haraka iwezekanavo kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanachuoni. Kwa sababu hakuwa mwenye kupewa ruhusa. Msingi ni kwamba alitakiwa kutekeleza ndani ya wakati wake.

Ama akila kwa sababu ya udhuru kama mfano wa hedhi, damu ya uzazi, maradhi, safari na nyudhuru zengine zinazomhalalishia kuacha kufunga, basi ni lazima kwake kulipa. Lakini hata hivyo si lazima kufanya hivo kwa haraka. Muhimu alipe kabla ya kuingia Ramadhaan nyingine. Lakini imependekezwa kwake kufanya haraka kulipa. Kwa sababu kufanya hivo ni kuharakisha kuitakasa dhimma. Jengine ndio salama zaidi kwa mja. Kunaweza kujitokeza vikwazo vya kumzuia kufunga kama maradhi na mfano wake.

Akichelewesha kulipa mpaka kukaingia Ramadhaan ya pili na wakati huohuo akawa na udhuru wa kuchelewesha, kwa mfano udhuru wake ukaendelea, basi ni lazima kwake kulipa baada ya Ramadhaan ya pili.

Akichelewesha mpaka Ramadhaan ya pili pasi na udhuru wowote, basi ni lazima, mbali na kulipa deni lake, amlishe masikini kwa kila siku moja iliyompita.

Si sharti wakati wa kulipa deni la Ramadhaan kufululiza. Inasihi kufululiza na kuachanisha. Amesema (Ta´ala):

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Hakushurutisha (Subhaanah) katika siku hizi kufululiza. Ingelikuwa ni sharti basi (Subhaanahu wa Ta´ala) angelibainisha.

[1] 02:184-185

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 162
  • Imechapishwa: 28/04/2020