Namna ya kumrejea mwanamke aliyeachika

Swali: Amempa mke wake talaka moja na kumepita miezi sita. Je, inajuzu kumrejea? Ni nini anatakiwa kufanya? Je, kumrudisha kunakuwa haramu au hapana?

Jibu: Ikiwa amemtaliki talaka moja tu, hii inaitwa talaka ya kurejea. Ana haki ya kumrudia mkewe muda wa kuwa bado yupo katika eda. Hapa ni pale ambapo ameshampa talaka moja tu na hakuna talaka nyingine kabla yake, na pia ikiwa tayari amemwingilia au aliishi naye faragha au alijamiiana naye. Hivyo talaka moja kama hii ni ya kurejea. Anayo ruhusa ya kumrudia hata baada ya miezi sita ikiwa bado hajatoka katika eda kwa sababu ya kuwa mjamzito au kwa sababu hedhi yake imechelewa na hajapata hedhi mara tatu. Basi anaweza kumrudia.

Lakini ikiwa tayari amepata hedhi mara tatu au amezaa ikiwa alikuwa mjamzito, basi anakuwa ameharamika kwake hadi kwa mkataba mpya wa ndoa. Kwa maana ya ndoa mpya kwa ridhaa yake na ridhaa ya walii wake, kama kwamba ni mgeni asiye na uhusiano naye. Akishatoka katika eda, hairuhusiwi kumrudia isipokuwa kwa ndoa mpya yenye masharti yote yanayotakiwa katika Shari´ah kama wanavyotakiwa wengine wote wanaotaka kumuoa. Lakini ilimradi bado yupo katika eda, iwe kwa sababu ya ujauzito ambao bado haujatoka, kwa sababu ya eda ya miezi mitatu kwa mwanamke asiyepata hedhi au kwa sababu ya kuchelewa kwa hedhi yake ambapo hupata hedhi mara moja kwa mwezi, hivyo hedhi ya tatu imechelewa. Katika hali hii, akimrudia kabla hedhi ya tatu haijamalizika na kabla hajaoga baada ya hedhi ya tatu, basi hakuna tatizo kwake kumrejea.

Swali: Je, inahesabiwa kuwa talaka?

Jibu: Ndiyo, inahesabika kuwa talaka.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1200/كيفية-مراجعة-المطلقة
  • Imechapishwa: 14/06/2026