Mwanamke mwenye kubakwa anataka kujiua

Swali: Nilisoma katika gazeti ”al-Mujtama´” wito kutoka kwa wanawake waislamu walioko magerezani katika moja ya nchi za Kiislamu. Wanawake hao waliomba waislamu wavunje na kulipua magereza na vituo vya kuwazuilia wafungwa, kwa sababu heshima zao zimekiukwa na hivi sasa baadhi yao ni wajawazito kutokana na zinaa waliyolazimishwa ndani ya magereza. Ni ipi hukumu ya kujiua katika hali kama hiyo na hukumu ya wanawake hao waliopata mtihani huo?

Jibu: Kujiua Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amekataza na vivyo hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا

“Wala msiziue nafsi zenu. Hakika Allaah ni Mwenye kuwahurumia.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha dhidi ya kujiua na akatoa khabari kuhusu mtu aliyepata maumivu makali ya jeraha kisha akajiua, akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Allaah (´Azza wa Jall) amesema: “Mja Wangu amejiharakisha Kwangu kwa nafsi yake na hivyo Nimeharamisha Pepo kwake.”

Kwa hiyo kujiua haijuzu. Haijuzu kwa mtu, hata akipatwa na mtihani, kujiua. Ikiwa ameumbiwa na maovu kama kufanyiwa machafu kwa la kulazimishwa au jambo jingine. Kwa hiyo haifai kujiua wala kwa sababu ya kufungwa. Bali anatakiwa ajilinde na ajitetee kadiri awezavyo. Vivyo hivyo mwanamume anaweza kujaribiwa kwa kulazimishwa kufanya liwati au mengineyo. Naye anatakiwa kujitetea kadiri ya uwezo wake, hata kama kuendelea kujitetea kutapelekea kuuawa. Lakini haijuzu yeye kujiua. Anatakiwa ajihami na asijiachie kuingiliwa kinyume na maumbile au kufanyiwa machafu mengine. Akifariki kwa kuuawa na mhalifu, basi yeye ni shahidi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuuawa kwa kutetea mali yake amekufa shahidi, mwenye kuuawa kwa kutetea dini yake amekufa shahidi na mwenye kuuawa kwa kutetea damu yake amekufa shahidi.”

Vilevile alimjia mtu akamwambia: ”Ee Mtume wa Allaah, mtu ananijia akitaka mali yangu?” Mtume akasema: ”Usimpe mali yako.” Akasema: ”Akinipiga vita?” Akasema: ”Pambana naye.” Akasema: ”Nikimuua?” Akasema: ”Yeye atakuwa Motoni.” Akasema: ”Akiniua?” Akasema: ”Wewe utakuwa Peponi.”

Hii ni dalili inayoonyesha kuwa mtu anayedhulumiwa anatakiwa kupigana na kujihami. Akinusurika basi mhalifu atakuwa Motoni. Asiponusurika na akauawa, basi ni kwa hekima kubwa ya Allaah na siri ambazo sisi hatuzijui. Yeye ni shahidi. Kwa mfano ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) – ambaye ndiye bora zaidi kuliko watu wote baada ya Abu Bakr as-Swiddiyq na baada ya Manabii – aliuliwa katika msikiti huku akiwa anawaongoza watu katika swalah, kwa hekima ya Allaah. Aliuliwa na kafiri mmoja aitwaye Abu Lu´lu´ah aliyekuwa mwabudia moto, kwa sababu ya hukumu ambayo ´Umar alimwekea. Kwa hiyo uuaji unaweza kuwapata watu wema au wasio wema. Mtu anaweza kuuawa kwa kuumbiwa kama walivyouwawa baadhi ya Manabii. Baadhi ya Manabii waliuawa ilihali wao ndio bora wa watu, kama Allaah alivyoeleza katika Qur-aan Tukufu kwamba mayahudi waliua Manabii wao bila haki. Vivyo hivyo baadhi ya watu wema kama ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy ambao waliuawa bila haki. Aidha az-Zubayr na Twalhah bin ´Ubaydillaah. Lengo ni kuwa aliyedhulumiwa na akauawa, jambo hilo linajulikana na yeye ni shahidi. Yule mhalifu atakuwa Motoni. Basi yeyote aliyepatwa na balaa katika nafsi yake anatakiwa ajihami, ajikaze na ajitetee. Akiweza kumuua mhalifu ili kuzuia uovu, basi amuue mhalifu. Lau mhalifu hatazuiliwa isipokuwa kwa kuuawa, basi amuue. Kama akizuiwa kwa maneno ya kumuonya kuhusu matokeo ya uhalifu, basi ni vyema. Asipoweza kuiziwa isipokuwa kwa kumuua kwa kumkaba au kumdunga kisu au njia nyingine yoyote, basi atafanya hivyo. Yeye hana lawama na mhalifu atakuwa. Ama akidhibitiwa na mhalifu akauawa, basi mtu huyo ni shahidi na atakuwa Peponi.

[1] 04:29

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1112/حكم-قتل-المسلم-نفسه-خوفا-من-التعذيب
  • Imechapishwa: 19/08/2026