Ibn Baaz kuhusu kumsomea Yaa Siyn anayetaka kukata roho II

Swali: Kusoma Suurah Yaa Siyn wakati wa kukata roho?

Jibu: Kusoma Yaa Siyn wakati mtu yuko katika hatua za mwisho za uhai imetajwa katika Hadiyth ya Ma´qil bin Yasaar, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

“Wasomeeni mauti wenu Yaa Siyn.”

Ibn Hibbaan na baadhi ya wanazuoni wameisahihisha na wakadhani kuwa cheni yake ya wapokezi ni nzuri na kwamba wakidhani kuwa imesimuliwa na Abu ´Uthmaan an-Nahdiy kutoka kwa Ma´qil bin Yasaar. Lakini wengine wameidhoofisha na kusema kuwa msimulizi si Abu ´Uthmaan an-Nahdiy, bali ni mtu mwingine asiyejulikana.

Kwa hivyo wanazuoni mashuhuri wa Hadiyth wamekubaliana kuwa Hadiyth hii ni dhaifu. Kwa hiyo haisuniwi kusomewa maiti Yaa Siyn. Wale waliopendekeza jambo hilo wamedhani kuwa Hadiyth ni Swahiyh ndio maana wakapendekeza kitendo hicho.

Hata hivyo kusomewa Qur-aan mgonjwa ni jambo lenye manufaa. Kusoma sehemu yoyote ya Qur-aan, bila kufanya Yaa Siyn kuwa maalum, kumletea mgonjwa unyenyekevu na utulivu na anaweza kunufaika, khaswa ikiwa bado anaelewa na kufahamu. Lakini kuifanya Yaa Siyn maalum kwa wakati huo hakuthibiti, kwa sababu cheni yake ya Hadiyth imeonekana kuwa dhaifu na hivyo hakuna msingi wa kuifanya maalum. Kusomewa Qur-aan kwa ujumla kwa mgonjwa ni vizuri na ni jambo lenye manufaa kwake na kwa wahudhuriaji.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1152/هل-يجوز-قراءة-يس-عند-الاحتضار
  • Imechapishwa: 19/08/2026