Mwanamke aliye ndani ya eda anataka kuhiji II

Swali 67: Je, inajuzu kwa mwanamke kutekeleza faradhi ya Hijjah akiwa katika eda baada ya kufiwa na mume wake au baada ya talaka?

Jibu: Ama kwa mwanamke aliyefiwa na mume wake, basi haijuzu kwake kutoka nyumbani kwake na kusafiri kwenda Hijjah mpaka amalize eda kwa sababu katika hali hii hana uwezo. Hiyo ni kwa sababu ni wajibu kwake kukaa nyumbani. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا

“Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, hao wake wangojee peke yao [eda ya] miezi minne na siku kumi.”[1]

Kwa maana nyingine ni lazima asubiri nyumbani kwake mpaka eda imalizike.

Ama mwanamke mwenye eda isiyokuwa ya kufiwa, basi aliyepewa talaka ya rejea hukumu yake ni kama hukumu ya mke. Kwa hivyo hasafiri isipokuwa kwa ruhusa ya mume wake. Lakini hakuna ubaya kwa mume ikiwa ataona maslahi ya kumpa ruhusa kwenda Hijjah na akahiji pamoja na Mahram wake. kuhusu mwanamke aliyepewa talaka isiyokuwa ya rejea, kilichowekwa katika Shari´ah kwake ni yeye kubaki nyumbani kwake pia. Lakini anaweza kuhiji ikiwa mume atakubaliana na hilo, kwa sababu mume ana haki katika kipindi hiki cha eda. Hivyo akimruhusu kuhiji hapana vibaya.

Kwa ufupi ni kwamba mwanamke aliyefiwa na mume wake ni wajibu kwake kubaki nyumbani na wala asitoke. Ama mwanamke aliyepewa talaka rejea, yeye yuko katika hukumu ya wake na hivyo jambo lake liko kwa mume wake. Ama aliyepewa talaka isiyokuwa ya rejea, yeye ana uhuru zaidi kuliko yule wa kurejewa. Lakini pamoja na hivyo mume wake ana haki ya kumzuia kwa ajili ya kulinda eda yake.

[1] 02:234

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (21/69-70)
  • Imechapishwa: 25/05/2026