3 – Kichenguzi cha tatu cha wudhuu´: Kutokwa na akili. Wudhuu´ unabatilika kwa kupoteza akili kwa sababu ya wazimu, ulevi, kupoteza fahamu au usingizi mzito. Ama ikiwa ni usingizi wa kutopepesa macho tu usioondoa hisia, mfano akiwa ameketi au amesimama, kisha akapatwa na usingizi na kichwa chake kikainama kisha akazinduka, basi jambo hili halichengui wudhuu´. Muslim amepokea katika ”as-Swahiyh” yake (376) kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wanalala kisha wanaswali bila ya kutawadha.”

Tamko lake lipo kwa Abu Daawud (200):

“Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakingoja swalah ya ´Ishaa ya mwisho mpaka vichwa vyao viinamie kwa usingizi, kisha wanaswali bila kutawadha.”

Hili linajulisha ya kwamba kuondokwa na akili sio hadathi, bali ni sababu ya kutia shaka kuwa kuna hadathi. Pia kinachofahamisha hilo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kufunga sehemu ya haja ni macho mawili. Hivyo basi anayelala na atawadhe.”

Ameipokea Abu Daawud (203) kupitia kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh). Cheni yake yake ya wapokezi ni nzuri. Tazama ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (113). Kumenukuliwa kwamba an-Nawawiy, al-Mundhiriy na Ibnus-Swalaah wameifanya kuwa ni nzuri.

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 25/05/2026