Swali: Ni wakati kiasi gani uliowekwa katika Shari´ah kati ya adhaana mbili; adhaana ya kwanza na ya pili ya ijumaa? Je, ni kama kitendo kinachofanywa na mji huu au ni kama kitendo kinachofanywa na Makkah na al-Madiynah?

Jibu: Ni nchi moja na wala si sahihi kupambanua kati yake. Qaswiym na Makkah na al-Madiynah ni nchi moja. Mimi nilidhani utasema nchi moja wapo ya Shaam kama ´Iraaq au nyengineyo. Kwa ajili hii jambo la kwanza anatakiwa kusahihisha ibara.

Uhalisia wa mambo ni kwamba hapa Najd tunapambanua kati ya adhaana ya kwanza na adhaana ya pili kwa nusu saa, saa moja n.k. Makkah na al-Madiynah hawapambanui kwa njia ya kwamba kunapoingia wakati wa swalah ya Dhuhr muadhini anaadhini adhaana inayoitwa kuwa ni ya kwanza. Kisha wanaadhini ya pili pale anapoingia Khatwiyb. Kile kinachonidhihirikia ni kwamba kitendo cha watu wa Najd ndio sahihi zaidi kwa sababu ndio kunapatikana kwacho faida. Watu wanasikia adhaana ya kwanza kisha wanajiandaa kwa ajili ya kwenda msikitini. Wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wamesema kwamba yule mwenye kusikia wito wa pili wa ijumaa basi ni lazima papo hapo ataposikia tu kuharakisha kwenda. Yule ambaye nyumba yake itakuwa mbali basi ni lazima kuharakisha kwenda katika ijumaa kwa njia ya kwamba afike pamoja na Khatwiyb. Kwa hivyo kile kitendo kinachofanywa na watu hapa – yaani Qaswiym – ndio kiko karibu zaidi na usawa kuliko wale ambao wanaadhini adhaana ya kwanza ya ijumaa pale kunapoingia wakati wa Dhuhr. Lakini hiyo haina maana kwamba tunawatia upotofuni wale wanaotofautiana na sisi. Hii ni nukta muhimu nawazindua kwayo wanafunzi. Wanachuoni wa Fiqh wakitofautiana katika masuala fulani ambapo baadhi wakasema kwamba ni Sunnah na wengine wakasema kuwa sio Sunnah, maoni ya wale wenye kusema kuwa sio Sunnah haina maana kwamba yanalazimisha wawe wameingia katika Bid´ah. Hawawafanyii Tabdiy´ kabisa. Kwa sababu iwapo tutawafanyia Tabdiy´ wale wanaotofautiana na sisi katika masuala haya, basi ni lazima Fuqahaa´ wote katika mambo ya tofauti wawe ni wazushi. Kwa sababu yule mwenye kunambia kuwa mimi ni mzushi na mimi nitamwambia kwamba ni mzushi pia. Matokeo yake Fuqahaa´ wote katika mambo ya tofauti wanakuwa ni Ahl-ul-Bid´ah, jambo ambalo halisemwi na yeyote. Wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wakitofautiana katika mambo yasiyohusiana na ´Aqiydah na sio mambo yaliyozuliwa ya waziwazi, bali wametofautiana katika kuyafahamu maandiko, basi hapa tunasema kuwa jambo ni lenye wasaa na hatuwezi kufanyiana Tabdiy´ sisi na sisi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (69) http://binothaimeen.net/content/1545
  • Imechapishwa: 26/07/2019