Mtu ambaye ameanza Hajj yake kwa ajili ya asiyekuwa Allaah

Swali: Vipi ikiwa mtu ameanza Hajj si kwa ajili ya Allaah, kisha ikamtokea kumtakasia nia Allaah akiwa ´Arafah au kabla ya kutufu?

Jibu: Kinachonidhihirikia ni kuwa ikiwa msingi wa Hajj yake ulikuwa si kwa ajili ya Allaah, basi ni lazima aikamilishe. Allaah amesema:

وَأَتِمُّوا الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ لِلَّـهِ

“Timizeni Hajj na ‘Umrah kwa ajili ya Allaah.“[1]

Lakini nia yake ikiwa ilikuwa si kwa ajili ya Allaah, basi thawabu yake inabatilika. Hatakuwa na malipo ya Hajj, bali atakuwa na dhambi; dhambi ya shirki ndogo.

Mwanafunzi: Je, ni wajibu aimalize ilihali msingi wa ´ibaadah yake ilikuwa si kwa ajili ya Allaah?

Ibn Baaz: Ndio, hata kama. Ameshalazimika kwa kuingia kwake humo. Dai lake kwamba alinuia hivi au vile halikubaliki. Lazima aimalize, kwa sababu Allaah Amesema:

وَأَتِمُّوا الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ لِلَّـهِ

“Timizeni Hajj na ‘Umrah kwa ajili ya Allaah.“

Mwanafunzi: Je, Aayah hii si inawahusu wale waliokusudia na wakaianza Hajj kwa ajili ya Allaah, kama pale ambapo Hajj inakuwa batili kwa jambo lililotokea wakati wa ´ibaadah, kama vile mtu aliyeanza kwa ajili ya Allaah kisha akafanya kitendo kama kujamiiana?

Ibn Baaz: Ikiwa aliianza si kwa ajili ya Allaah, jambo hili linahitaji kutafakari zaidi.

[1] 02:196

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/31360/ما-حكم-من-ابتدا-الحج-بنية-لغير-الله
  • Imechapishwa: 22/10/2025