Swali: Je, kusoma kwa ajili ya kupata cheti kunahesabiwa kuwa ni shirki? Kama ni shirki, je, ni shirki kubwa au ndogo?

Jibu: Inampasa muumini masomo yake yawe kwa lengo la kupata ufahamu wa dini na kujifunza na kujua yale ambayo Allaah ameamrisha na aliyokataza ili awe na uelewa sahihi. Lakini akijisomea kwa ajili ya dunia tu, hilo ni miongoni mwa shirki ndogo. Mtu anapaswa nia yake iwe ni kutafuta radhi za Allaah na Pepo ya Aakhirah. Juhudi zake ziwe za juu. Wanazuoni wamesema katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd”:

”Mlango unaozungumzia kwamba miongoni mwa shirki ni mtu kutaka dunia kwa matendo yake.”

Kwa hiyo muumini anapaswa kuwa na nia ya juu, akikusudia katika masomo yake uso wa Allaah na makazi ya Aakhirah, si ulimwengu na starehe zake. Muumini ameamrishwa awe mwenye kumtakasia nia Allaah pekee. Amesema (Ta´ala):

فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ

”Mwabudu Allaah kwa kumtakasia dini Yeye, Zindukeni! Ni ya Allaah pekee dini iliyotakasika.”[1]

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini.”[2]

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

“Hivyo anayetaraji kukutana na Mola wake na atende matendo mema na wala asishirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote!”[3]

Kwa hiyo anayejifunza, akaamrisha mema au kukemea maovu kwa ajili ya dunia, na si kwa ajili ya Allaah, huyo ametumbukia katika shirki ndogo. Huo ni msiba mkubwa.

[1] 39:2-3

[2] 98:5

[3] 18:110

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/31693/هل-تعتبر-الدراسة-من-اجل-الشهادة-شركا
  • Imechapishwa: 18/12/2025