Swali: Ni ipi hukumu ya picha?

Jibu: Ni jambo linalojulikana kwamba picha ni haramu. Lakini pindi kitu kinapokuwa cha kawaida basi hupotea ukhatari wake. Pindi mtu anaposema kuwa picha ni haramu, basi watu husema kuwa anaishi katika zama za kale, kwa sababu ni wajinga juu ya Shari´ah ya Mtume wao na Uislamu. Wamezowea kutazama picha asubuhi na jioni. Hata hivyo kumepoklewa Hadiyth nyingi ambazo zote zinaharamisha picha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila mtengeneza picha ni katika Motoni. Ataijaalia kila picha aliyotengeneza roho aadhibiwa kwayo Motoni.”[1]

“Hakika watu wenye adhabu kali siku ya Qiyaamah ni wale wanaoigiliza uumbaji wa Allaah.”[2]

Hizi zinafahamisha kwamba picha ni haramu. Baadhi wanasema kuwa picha zilizo za haramu ni zile za kiwiliwili ama zile za kamera sio haramu. Hili ni kosa. Hadiyth ilioko kwa Muslim inafahamisha kuwa zote ni haramu. Picha za kiwiliwili haitoshi kuziharibu peke yake bali inatakiwa vilevile kuzitokomeza na kuzivunja. Kwa mujibu wa Imaam an-Nawawiy ni kwamba maimamu wanne wote wameafikiana juu ya uharamu wa picha aina zote, ni mamoja ni zile zenye kivuli au hazina kivuli. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh)  amesema:

“Ikiwa unalazimika kutengeneza, basi fanya zile zisizokuwa na roho.”

Hayo ndio maoni walionayo pia Hanaabilah; wanajuzisha zile picha za viumbe visivyokuwa na roho. Hadiyth zinajulisha kuwa ni haramu kutengeneza picha ya viumbe vyenye roho, kama alivosema Ibn ´Abbaas pia.

[1] Muslim (2110).

[2] al-Bukhaariy (5954) na Muslim (2107).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin Humayd
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Ibn Humayd, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 30/05/2021