Mke anamtaka mume alipe deni lake la dhahabu baada ya miaka 15 iliyopita

Swali: Nilichukua dhahabu ya mke wangu na nikaiuza kwa ridhaa yake kamili kwa shida iliyonipata tangu miaka kumi na tano iliyopita. Thamani ilikuwa deni juu yangu kwake. Sasa baada ya kupanda bei ya dhahabu mara kumi, ananitaka nimlipe kwa thamani ya sasa au nimrudishie uzito wa dhahabu yake. Nifanye nini ili nijitoe katika dhimma ya deni hili?

Jibu: Ni juu yako kumrudishia dhahabu yake ikiwa alikupa dhahabu na akakuruhusu uiuze na uitumie katika haja zako. Dhahabu inahesabiwa kuwa ni mkopo juu yako, uzito kwa uzito. Ikiwa uliiuza kwa hesabu yake na akakubali kuwa mkopo ni thamani, basi juu yako ni kurudisha thamani. Ama ikiwa mkopo uliopo baina yako na yeye ni ileile dhahabu kwamba umrudishie mfano wa dhahabu yake, basi Waislamu wako juu ya masharti yao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Waislamu wako juu ya masharti yao.”

Ikiwa ulikubaliana naye kwamba utamrudishia dhahabu yake, basi mrudishie mfano wa dhahabu yake, ni mamoja iwe ni ghali au nafuu. Ikiwa lililofanyika baina yako na yeye ni kwamba unaiuza dhahabu kwa hesabu yake na kwamba thamani inakuwa juu yako kwake, basi waislamu wako juu ya masharti yao. Kwa maana katika masharti yake ni pia thamani.

Lililo bora kwako, ee ndugu yangu, ni kumpa kile kitakachomridhisha, hiki au hiki. Kwa sababu mgogoro baina yenu unaweza kupelekea yale ambayo mwisho wake si mzuri. Kwa hiyo nasaha yangu kwako ni kumpa kile kinachomridhisha, hata kama kuna uzito juu yako. Hili ndilo lenye kufaa zaidi kwako. Hakika amekufanyia wema na akakufanyia wasaa, basi mridhishe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika bora ya watu ni wale walio bora zaidi katika kulipa.”

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3482/كيفية-القضاء-لمن-استدان-من-امراته-ذهبا
  • Imechapishwa: 31/08/2026