Mgonjwa anasema hataki kujitibisha kwa kutaraji malipo kwa Allaah

Swali: Nina ndugu yangu katika dini aliyepatwa na maradhi makali. Nikamwambia aende kwa daktari apate tiba upone – kwa idhini ya Allaah. Akasema kuwa anamshukuru Allaah ambaye amemtosheleza kutokana nao na kwamba Allaah ameweka katika ugonjwa huu malipo makubwa na hilo linamtosha. Je, yuko sahihi au amekosea?

Jibu: Hakuna ubaya kwake. Kuacha dawa inajuzu. Lakini kilicho bora zaidi kwake ni kutafuta tiba. Na pia akisubiri juu ya maradhi kwa ajili ya kutafuta malipo, basi hakuna ubaya. Hata hivyo lililo bora zaidi na lenye kipaumbele ni atumie dawa na ajitibu, kwa sababu kufanya sababu ni jambo lililowekwa katika Shari´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alijitibu na Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walijitibu – nao ndio watu bora zaidi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila ugonjwa una dawa. Inapopatikana dawa inayopatana na ugonjwa, hupona kwa idhini ya Allaah.”

Na pia amesema:

“Allaah hakuteremsha ugonjwa wowote isipokuwa ameteremsha dawa yake.”

Hizi ni sababu. Huenda mgonjwa akapona kwa kutumia sababu hizo na huenda asipone kwa sababu muda wake umefika. Ikiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametaka apone, atamfanyia sababu ya kupona. Ikiwa mauti yamekaribia na muda wake umefika, basi sababu hazitamnufaisha na kila kitu kitakuwa kimekwisha.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3439/حكم-ترك-المداواة-بالعلاج-طلبا-للاجر
  • Imechapishwa: 22/08/2026