Swali 1: Ni ipi hukumu ya dini ya Kiislamu juu ya kuyatembelea makaburi, kufanya Tawassul kwa makaburi, kupokea kondoo na mali kwa ajili ya kufanya Tawassul kwayo kama kumtembelea bwana al-Badawiy, al-Husayn na bibi Zaynab?

Jibu: Kuna aina mbili za kuyatembelea makaburi:

Ya kwanza: Matembezi yaliyosuniwa na yanayotakikana kwa ajili ya kuwaombea du´aa wafu, kuwaombea rehema, kukumbuka Aakhirah na kujiandaa kwa ajili ya Aakhirah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yatembeleeni makaburi! Kwani hakika yanakukumbusheni Aakhirah.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pia alikuwa akiyatembelea. Vivyo hivyo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Hii ni aina kwa wanamme peke yao na hapana wanawake. Ama wanawake haikusuniwa kwao kuyatembelea makaburi. Bali ni lazima kuwakatalia jambo hilo. Kwa sababu imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amewalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi. Jengine ni kwa sababu wao kuyatembelea makaburi kunaweza kupelekea wakafitinisha au wakafitinishwa ukiongezea na uchache wa subira na wingi wa huzuni ambao huwapata.

Vivyo hivyo haikusuniwa kwao kuyasindikiza majeneza kwenda makaburi. Hilo ni kutokana na yale yaliyothibiti katika ”as-Swahiyh” kupitia kwa Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyeeleza:

”Tulikatazwa kuyasindikiza majeneza na wala hatukutiliwa mkazo.”

Hilo limejulisha kwamba wamekatazwa kuyasindikiza majeneza kwenda makaburini. Ni kutokana na yale yanayokhofiwa kwa jambo hilo katika kufitinisha na kufitinishwa na uchache wa subira. Kimsingi makatazo yanapelekea katika uharamu. Kutokana na maneno ya Allaah (Subhaanah):

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni.”[1]

Kuhusu kumswalia maiti ni jambo limesuniwa kwa wanamme na wanawake. Kama zilivyosihi Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutoka kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) juu ya jambo hilo. Kuhusu maneno ya Umm ´Atwiyyah:

”… wala hatukutiliwa mkazo.”

si jambo linalojulisha kwamba inafaa kwa wanawake kuyasindikiza majeneza. Kwa sababu kitendo chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kukataza kinatosha juu ya kukataza. Kuhusu maneno yake:

”… wala hatukutiliwa mkazo.”

yamejengeka juu ya Ijtihaad na dhana yake. Ijtihaad yake haiwezi kupingana na Sunnah.

Ya pili: Bid´ah. Mtu akayatembelea makaburi kwa ajili ya kuwaombea du´aa watu wake, kuwataka msaada, kuwachinjia au kuwawekea nadhiri. Huu ni uovu na shirki kubwa. Kunaingia pia mtu akayatembelea kwa ajili ya kuwaomba du´aa, kuswali na kusoma Qur-aan karibu nayo. Hii ni Bid´ah ambayo haikuwekwa katika Shari´ah. Pia ni katika njia za shirki. Uhakika wa mambo ni kwamba ni aina tatu:

1- Matembezi yaliyowekwa katika Shari´ah. Akayatembelea kwa ajili ya kuwaombea watu wake au kwa ajili ya kukumbuka Aakhirah.

2- Mtu akayatembelea kwa ajili ya kusoma Qur-aan, kuswali au kuchinja karibu nayo. Hii ni Bid´ah na ni miongoni mwa njia zinazopelekea katika shirki.

3- Mtu akayatembelea kwa ajili ya kuwachinjia wafu, kujikurubisha kwao, kuwaomba wafu badala ya Allaah, kuwataka uokozi, msaada au nusura. Hii ni shirki kubwa.

Ni lazima kutadhari kutokamana na matembezi haya yaliyozuliwa. Hakuna tofauti kwamba yule mwombwaji ni Mtume, mja mwema au mtu mwingine.

Kunaingia katika hao yale yanayofanywa na baadhi ya wajinga kwenye kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kumuomba na kumtaka msaada au kwenye kaburi la al-Husayn, al-Badawiy, Shaykh ´Abdul-Qaadir al-Jaylaaniy au wengineo. Allaah ndiye mwenye kutakwa msaada.

[1] 59:07

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Akhtwaau fiyl-´Aqiydah, uk. 6
  • Imechapishwa: 04/08/2020