Swali: Je, matabano yanapingana na utegemezi?

Jibu: Utegemezi wa kweli ni ule ukweli wa kumtegemea Allaah katika kufikia manufaa na kuzuia madhara pamoja na kufanya sababu ambazo Allaah ameamrisha. Utegemezi sio kumtegemea Allaah bila ya kufanya sababu, bali kufanya hivo ni kumtukana Allaah (´Azza wa Jall) na hekima Yake, kwa sababu  Allaah (Ta´ala) ameyafungamanisha matokeo na sababu zake.

Ni mtu gani ambaye alikuwa akimtegemea Allaah zaidi? Ni Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Je, alikuwa akifanya sababu anazoepuka kwazo madhara? Ndio alikuwa akifanya hivo. Wakati anapotoka kwenda vitani  alikuwa akivaa silaha kwa ajili ya kujikinga na mishale. Katika vita vya Uhud alivaa ngao mbili kwa lengo la kujilinda. Kwa hivyo kufanya sababu hakupingani na utegemezi ikiwa mtu anaitakidi kuwa hiyo ni mbinu tu ambayo haisaidii isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Kutokana na hayo mtu kujifanyia matabano mwenyewe au akawatabana ndugu zake wengine ambao ni wagonjwa hakupingani na kumtegemea Allaah. Hakika imethibiti kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitabana mwenyewe kwa Suurah “al-Falaq” na “an-Naas” na pia akiwafanyia matabano Maswahabah wake wanapokuwa wagonjwa – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/64-65)
  • Imechapishwa: 28/06/2026