Swali: Ni ipi hukumu ya matabano? Ni ipi hukumu ya kuandika Aayah za Qur-aan na kuzitundika kwenye shingo ya mgonjwa?

Jibu: Inafaa kumtabana aliyefanyiwa uchawi au magonjwa mengine ikiwa ni katika Aayah za Qur-aan tukufu au du´aa zinazoruhusiwa. Imethibiti kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwafanyia matabano Maswahabah zake. Miongoni mwa aliyokuwa akiwafanyia matabano kwayo ni pamoja na:

“Yule ambaye atahisi maumivu mmoja wenu, au akahisi maumivu ndugu yake, aseme: “Mola wetu ni Allaah ambaye yuko mbinguni. Limetakasika jina Lako. Amri Yako iko mbinguni na ardhini kama ambavyo huruma Yako iko mbinguni. Tusamehe madhambi na makosa yetu. Wewe ni Mola wa wazuri. Teremsha rehema Yako na dawa Yako kwa huyu anayehisi maumivu.” ili aweze kupona.”[1]

Miongoni mwa du´aa zilizosuniwa ni pamoja na:

بِسْمِ اللَّهِ أَرْقِيكَ، مِنْ كُلِّ شَيْءٍ يُؤْذِيكَ، مِنْ شَرِّ كُلِّ نَفْسٍ أَوْ عَيْنِ حَاسِدٍ، اللَّهُ يَشْفِيكَ، بِسْمِ اللَّهِ أَرْقِيكَ

“Naanza kukusomea kwa jina la Allaah, kutokamana na kila kitu chenye kukuudhi, na kutokamana na shari za kila nafsi au kijicho hasidi Allaah akuponye. Naanza kukusomea kwa jina la Allaah.”[2]

Aidha ni sawa kuweka mkono wake katika kile kiungo kinachomuuma na kusoma:

بِسْمِ اللَّهِ، أَعُوذُ بِاللَّهِ وَقُدْرَتِهِ مِنْ شَرِّ مَا أَجِدُ وَأُحَاذِرُ

“Najilinda kwa Allaah na kwa uwezo Wake kutokamana na shari ya ninachokihisi na ninachokitahadhari nacho.”[3]

Kuhusu hirizi za Qur-aan na Adhkaar, wanazuoni wamekinzana juu ya hilo; baadhi wamejuzisha jambo hilo na wengine wamelikataza. Maoni sahihi zaidi ni kwamba inakatazwa kwa sababu jambo hilo halikupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo kilichopokelewa ni kumsomea mgonjwa[4]. Ama kutundika hirizi juu ya shingo au mkononi mwa mgonjwa au chini ya mito yake na mfano wa hayo, kwa mujibu wa maoni yenye nguvu zaidi ni kwamba mambo hayo yamekatazwa kwa sababu ya kutokuwepo dalili juu ya mambo hayo. Kila mtu ambaye anafanya jambo kuwa ni sababu pasi na idhini kutoka katika Shari´ah, basi kitendo chake hicho kinazingatiwa ni aina fulani ya shirki. Kwa sababu ni kukithibitishia kitu sababu ambacho Allaah hakukifanya kuwa ni sababu.

[1] Abu Daawuud (3892), an-Nasaa’iy (10877) na al-Haakim (1/344). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Sunan Abiy Daawuud” (3892).

[2] Muslim (2186).

[3] Abu Daawuud (3891). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (3891)).

[4] al-Bukhaariy (5748).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/63-64)
  • Imechapishwa: 28/06/2026