Kuhusiana na Allaah kuonekana duniani hali ya kuwa mtu yuko macho, hapa ndipo watu wamezozana:

Mushabbihah wanaonelea kuwa Allaah anaonekana duniani na kwamba anahudhuria, anacheza shere, anapeana mikono, anakumbatiana na anateremka mchana wa ´Arafah akiwa juu ya ngamia. Allaah awafedheheshe. Mushabbihah hawa ni wale Shiy´ah waliopitiliza. Ni makafiri. Wanasema kuwa Allaah yuko katika umbile la mwanaadamu na kuwa anafanana na mwanaadamu katika sifa Zake. Allaah awafedheheshe.

Kadhalika baadhi ya Suufiyyah wamesema kuwa Allaah anaweza kuwa kwa rangi ya manjano. Ukiona kitu cha manjano wanasema kwamba kuna uwezekano Allaah akawa kwenye manjano hayo. Allaah awafedheshe.

Mbali na Mushabbihah hawa Ummah mzima umekubaliana juu ya kwamba Allaah (Ta´ala) hakuna yeyote awezae kumuona duniani. Hawakutofautiana katika hilo isipokuwa kuhusiana na Mtume Wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wametofautiana kuhusiana na kama alimuona Mola Wake usiku wa Mi´raaj au hakumuona. Upande mwingine wakakubaliana juu ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuona Mola Wake ardhini. Hili ni kwa maafikiano. Vilevile wakakubaliana juu ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola Wake kwa macho ya moyo wake na si kwa macho ya kichwa chake. Makusudio ya kumuona kwa macho ya moyo wake ni elimu zaidi juu ya elimu ya kawaida. Kitu ambacho wanachuoni wametofautiana nacho ni kama Mtume alimuona Mola Wake kwa macho ya kichwani mwake usiku wa Mi´raaj mbinguni. Hili lina kauli tatu zifuatazo:

1- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola Wake kwa macho ya kichwani mwake usiku wa Mi´raaj tu. Hili limepokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas na wenzake. Vilevile kuna upokezi mmoja kutoka kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) na Imaam an-Nawawiy amechagua kauli hii katika kitabu chake “Sharh Swahiyh Muslim”. Kadhalika ameichagua Abul-Hasan al-Ash´ariy na wenzake, Imaam Muhammad bin Ishaaq bin Khuzaymah katika “Kitaab-ut-Tawhiyd” na Abu Ismaa´iyl al-Harawiy. Wote hawa wanaonelea kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola Wake kwa macho ya kichwani mwake usiku wa Mi´iraaj. Wametumia dalili kwa maneno ya Allaah (Ta´ala):

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Utakasifu ni wa ambaye amemsafirisha mja Wake usiku kutoka al-Masjid al-Haraam mpaka al-Masjid al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake [amechukuliwa] ili Tumuonyeshe baadhi ya ishara Zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (17:01)

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba amesema kuwa ni muonekano wa macho ambao alioneshwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usiku aliyosafarishwa . Imaam Muhammad bin Ishaaq bin Khuzaymah amepokea hilo katika kitabu “Kitaab-ut-Tawhiyd” na wengine.

2- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuona Mola Wake kwa macho ya kichwani mwake usiku wa Mi´raaj. Bali alimuona kwa macho ya moyoni mwake. Hili limepokelewa kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kumwambia Masruuq wakati alipomuuliza:

“Je, Muhammad alimuona Mola Wake?” Akasema: “Nywele zangu zimesisimka kutokana na uliyoyasema.” Kisha akaendelea kusema: “Mwenye kukueleza kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemuona Mola Wake amesema uongo.” al-Bukhaariy (4855) na Muslim (177).

Katika upokezi mwingine amesema:

“Mwenye kudai kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemuona Mola Wake, amezua uzushi mkubwa kwa Allaah.” al-Bukhaariy (3234) na Muslim (177).

Haya yamepokelewa pia kutoka kwa Ibn Mas´uud, Abu Hurayrah na wakatofautiana kwalo jopo la Maswahabah na Taabi´uun. Hii ndio kauli ya wanachuoni wengi wa Fiqh na wa Hadiyth na wanafalsafa. Bali hii ndio kauli ya wanachuoni wengi. Hii ndio kauli sahihi kama itakavyokuja huko mbeleni…

3- Hawa ni wale waliosimama, bi maana hawakusema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola Wake kwa macho ya kichwani mwake kama ambavyo hawakusema vilevile hakumuona. Haya ndio maoni ya al-Qurtwubiy (Rahimahu Allaah) na al-Qaadhwiy ´Iyaadhw na wengine. Wamesema wamefanya hivo kwa sababu dalili ziko sawa sawa na masuala haya hamna ndani yake dalili yenye kukata mashauri moja kwa moja. Waliyotolea dalili makundi yote mawili udhahiri wake wamefanya hivo kwa kuegemea katika tafsiri. Hii ndio sababu iliyowafanya kusimama katika masuala haya.

Sahihi kuhusiana na masuala haya ni kundi lililo na kauli ya pili. Nayo ni ile yenye kusema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuona Mola Wake kwa macho ya kichwani mwake. Dalili walizotumia ziko wazi kabisa.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/246-251)
  • Imechapishwa: 27/05/2020