Mambo matatu muhimu yanayohusiana na swalah ya kupatwa kwa jua

Swali: Tunataka utubainishe hukumu zifuatazo katika swalah ya kupatwa kwa jua:

1- Ni kwa kitu gani mtu anazingatiwa kuwa amewahi swalah ya kupatwa kwa jua?

2- Je, Khutbah ya kupatwa kwa jua imewekwa katika Shari´ah kwa kila mtu?

3- Je, imamu aitoe akiwa amesimama au amekaa?

Jibu: Rak´ah ya kupatwa kwa jua inawahiwa kwa kuwahi ile Rukuu´ ya kwanza. Kwa mfano umekuja na imamu amekwishaenda Rukuu´ ya kwanza kisha ukajiunga naye anasoma halafu akaenda Rukuu´ ya pili, basi hii Rak´ah imekupita. Kwa sababu imamu amerukuu Rukuu´ mbili na wewe umewahi Rukuu´ moja tu. Kwa hivyo Rak´ah imekwishakupita. Kidhibiti ni kwamba pale utapojiunga pamoja na imamu baada ya Rukuu´ ya kwanza katika Rak´ah basi Rak´ah imekwishakupita.

Ikiwa utasimama ili uilipe unatakiwa kuikidhi kwa Rukuu´ moja au Rukuu´ mbili? Unatakiwa kuilipa kwa Rukuu´ mbili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yale mtakayowahi swalini na yale yaliyokupiteni yakamilisheni.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… yakidhini.”

Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa kila mmoja kukhutubu? Yule ambaye ana uwezo wa kuwanasihi watu basi azungumze. Imamu akiwa hawezi kuwakhutubia watu na kuwanasihi, basi asimame mmoja katika watu ambaye anaweza kufanya hivo na awakhutubia watu.

Je, awakhutubie hali ya kuwa amesimama? Ndio, anatakiwa kuwakhutubia akiwa amesimama. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoa Khutbah katika swalah ya kupatwa kwa jua hali ya kusimama. Hii ni dalili ya wazi inayofahamisha kwamba kutoa Khutbah ni jambo limewekwa katika Shari´ah na sio kwamba ni jambo lililotokea tu. Bali ni Khutbah iliyothibiti. Kila ambapo watu wataswalishwa swalah ya kupatwa kwa jua basi mtu anatakiwa kuwatolea Khutbah. Lakini hili ni kwa yule mwenye kuweza. Ama kuhusu yule asiyejua asizungumze. Akiwa hajui basi amtafute mmoja katika wanafunzi msikitini  na amuombe azungumze.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (72) http://binothaimeen.net/content/1647
  • Imechapishwa: 03/04/2020