Swali 99: Wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wameigawanya kufuru ya kimatendo mafungu mawili; kubwa na ndogo. Swali langu nilikuwa nauliza kuhukumu kinyume na aliyoteremsha Allaah ni katika aina kubwa au ndogo? Ni ipi dalili ya hayo kutoka katika Qur-aan na Sunnah?

Jibu: Mambo haya yamewekwa wazi na kubainishwa katika maneno ya wanachuoni wa Ummah; kwamba yule mwenye kuhukumu kinyume na aliyoteremsha Allaah hali ya kuitakidi kwamba jambo hilo linajuzu, kwamba ndio bora kuliko hukumu ya Allaah, ni sawa na hukumu ya Allaah na kwamba yuko na khiyari akitaka anaweza kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah na akitaka anaweza kuhukumu kwa hukumu nyingine, huyu ni kafiri kwa maafikiano.

Ama iwapo anaitakidi kwamba lililo la wajibu ni kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah (´Azza wa Jall) , kwamba ndio ya haki na kwamba kuhukumu kwa kingine ni batili, lakini hata hivyo amehukumu kwa hayo kwa sababu ya rushwa, kwa sababu ya matamanio ndani ya nafsi yake katika masuala fulani miongoni mwa masuala ambapo amekwenda kinyume na Shari´ah ya Allaah kwa kukusudia katika masuala fulani miongoni mwa masuala kwa sababu ya lengo miongoni mwa malengo – ima amefanya hivo kwa sababu ya matamanio ndani ya nafsi yake, kwa sababu ya kupokea rushwa, kutaka kumpaka mafuta mtu fulani – basi hiyo ni dhambi kubwa. Lakini pamoja na hivyo haimpeleki katika ukafiri. Kwa sababu anaamini uharamu wa hilo, kwamba ni mwenye kukosea na kwamba ni mwenye kwenda kinyume. Hiyo inakuwa dhambi kubwa. Huu ndio upambanuzi katika masuala haya.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa ´Ulamaa-ul-Kibaar fiy al-Irhaab wat-Tadmiyr, uk. 272
  • Imechapishwa: 18/10/2019