Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

07- Abu Ruqayyah Tamiym bin Aws ad-Daariy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Dini ni nasaha.” Tukauliza: “Kwa nani?” Akasema kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, kwa Viongozi wa Waislamu na watu wa kawaida.”

Nasaha kwa Allaah:

1- Ni neno la kijumla la kutimiza haki za Allaah (Jalla wa ´Alaa) zilizo za wajibu na zilipendekezwa. Haki za Allaah zilizo za wajibu:

a) Uola Wake: Kuamini kuwa Yeye Mola Pekee ndiye mwendeshaji ulimwengu huu. Hana mshirika katika Uola Wake na kuendesha Kwake mambo. Alilolitaka lilikuwa na kile asichokitaka hakikuwi. Anahukumu Akitakacho na Anafanya Akitakacho (Subhaanahu wa Ta´ala).

b) Uungu Wake: Amuabudu Yeye pekee kwa aina zote za ´ibaadah. Asimfanyie yeyote kitu miongoni mwa ´ibaadah isipokuwa Yeye Pekee (Subhaanahu wa Ta´ala). Kila ´ibaadah anayofanyiwa mwingine asiyekuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) ni jambo linatoka nje katika nasaha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), bi maana ni kutoka katika kutekeleza haki ambayo ni ya Kwake (Jalla wa ´Alaa).

c) Majina na Sifa Zake: Kuamini ya kwamba Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ana majina mazuri mno na sifa kuu na kwamba Hana mwenza wala mshirika. Allaah (Ta´ala) Amesema:

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua [mwengine] mwenye jina Lake?” (19:65)

لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ

“Hakuzaa na wala hakuzaliwa.” (112:03)

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

Muislamu aitakidi kuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) Ana yale Aliyojithibitishia Mwenyewe miongoni mwa majina mazuri mno na sifa kuu. Hana mwenza katika majina na sifa Zake.

Kuvuka mipaka katika mlango wa sifa kwa kufananisha sifa za Allaah na za viumbe ni kutoka nje ya nasaha ilio ya wajibu. Vilevile kuziharibu sifa za Allaah ni kutoka nje ya nasaha ilio ya wajibu.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Arba´iyn an-Nawawiyyah, uk. 59-160
  • Imechapishwa: 10/05/2020