Lengo la kuchinja katika ´Iyd-ul-Adhwhaa ni kwa sababu ya kunufaika na ile nyama yake ni dhana pungufu yenye kutokana na ujinga. Lengo la kuchinja ni kumwabudu Allaah (Ta´ala). Amesema (Ta´ala):

لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ

”Haimfikii Allaah nyama zake wala damu yake, lakini unamfikia uchaji kutoka kwenu.”[1]

Nimependa kuzindua juu ya hilo ni kwa sababu baadhi ya ndugu zetu wenye hisia na huruma wamekuwa wenye kutuma pesa kwenda katika miji  ya kimasikini ya waislamu ili wachinje huko. Haya ni kutokana na ujinga, upungufu na uoni wao mfupi. Kwa sababu kuchinja lengo ni kule kumwabudu Allaah kwa kichinjwa hicho. Ukishamchinja mnyama wako basi mpe yule unayemtaka nchini mwako na nje yake. Haifai kufanya hivo kabla ya kuchinja. Usichinje isipokuwa ndani ya mji wako. Bora zaidi ni kuchinja ndani ya nyumba yako ili familia yako wapate kuona kitendo hicho na waone nembo hii tukufu.

Kutuma pesa za kichinjwa ili wachinje nje ya nchi kitendo hicho kinapelekea kukosa manufaa na khatari. Manufaa unayokosa ni kudhihiri kwa nembo hii tukufu. Pengine miaka itakavyozidi kwenda jambo hili litasahaulika na pesa zitakuwa zinatumwa katika miji ya waislamu na matokeo yake miji ya waislamu itakuwa inakosa nembo hii tukufu. Jambo jengine linalompita mtu ni kwamba mtu ameamrishwa kuchinja kwa mkono wake na ataje jina la Allaah juu kichinjwa hicho, jambo ambalo linampita.

[1] 22:37

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa´-ul-Baab al-Maftuuh (04/228)
  • Imechapishwa: 18/07/2020