Swali: Inajuzu kwa imamu kuwaondoa katika safu watoto walio chini ya miaka saba?

Jibu: Haijuzu kwa imamu wala asiyekuwa imamu kuwaondoa wadogo kutoka katika safu. Isipokuwa ikiwa katika hilo kuna madhara kwa mfano wanapiga fujo, wanazunguka kati ya safu na mfano wa hayo. Katika hali hiyo ndio awaondoe. Lakini jambo la kwanza analotakiwa kufanya ni yeye kumfungamanisha mtoto huyo na mlezi wake aliyeko msikitini na kumweleza alichofanya na kwamba anapata dhambi kwa kule kumnyamazia. Ama mtoto asipofanya kitu asimwondoe. Bali watoto wanatakiwa kubaki sehemu zao. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayetangulia katika yale ambayo hakutangulia yeyote basi yeye ndiye mwenye haki zaidi napo.”

Ama maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wawe nyuma yangu kati yenu wakomavu na wenye akili.”

Wanaokusudiwa ni wale wenye busara na waliobaleghe wawe ndio watakaomfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni kweli kwamba endapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angelisema:

“Wasiwe nyuma yangu isipokuwa wakomavu na wenye akili.”

Hapo ndipo tungelisema tuwaondoe wadogo katika safu. Lakini alisema kwa njia ya kuamrisha na sio ya kukataza. Ameamrisha hawa wenye busara na werevu ndio watangulia ili wawe nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Isitoshe ni kwamba kuwafukuza wadogo ni jambo lina taathira katika nafsi zao; huwachukia wale wenye kuwafukuza, kuichukia misikiti, kuchukia mkusanyiko na ni jambo linalowaathiri huko mbeleni. Mdogo hasahau. Kwa mfano wewe kumbuka ulipokuwa mdogo na akakupiga mtu husahau.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (74) http://binothaimeen.net/content/1731
  • Imechapishwa: 26/08/2020