Kuwakemea watawala mbele ya umati wa watu ni katika mfumo wa Salaf?

Swali 24: Kuwakemea watawala mbele ya umati wa watu ni katika mfumo wa Salaf?

Jibu: Ukemeaji mbele ya umati wa watu kwa namna tunayoitambua linatokamana na mapinduzi ya Ibn Sabaa´ na wanafunzi zake, ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewasifu kuwa ni wanafiki[1]. Waislamu wamewaita kuwa ni ”Khawaarij”. Ni kosa kukataza maovu kwa njia hii ya kichochezi na ya kimapinduzi. Hawakatazi maovu isipokuwa juu ya mimbari kuanzia wakati wa Ibn Sabaa´ mpaka hii leo. Njia hii sio kuamrisha mema na kukataza maovu. Hakika si vyenginevyo kitendo hicho chenyewe ndio maovu makubwa zaidi kuliko maasi ambayo wanasema eti wanayatibu. Kitendo cha kukemea maovu juu ya mimbari na kuwachochea watu juu ya mapinduzi ni jambo ovu na baya zaidi kuliko maasi yalioko. Dalili ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuamrisha jambo hilo. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kufanya subira. Zayd bin Wahb amepokea kuwa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Baada yangu kutakuwepo na mapendeleo na mambo ambayo hamtoyatambua.” Wakasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Ni kipi unachotunasihi tukikutana na hali hiyo?” Akasema: ”Tekelezeni haki inayokuwajibikieni na mumuombe Allaah haki yenu.”[2]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Yeyote atakayeona kwa kiongozi wake kitu anachokichukia basi asubiri. Kwa sababu yeyote anayeacha mkusanyiko kwa kiasi cha shibiri akafa, basi amekufa kifo cha kipindi kabla ya kuja Uislamu.”[3]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ni shujaa na mwenye kututakia kheri, hatuamrishi woga, kushindwa wala kufanya mapinduzi. Anatuamrisha kufanya subira za kimantiki ambayo inaleta matunda mazuri duniani na Aakhirah. Watu hawa hawapandi isipokuwa shari na fitina. Hakuna kinachoweza kuvunwa na ummah kutokana na njia hizi za kimapinduzi za Ibn Sabaa´, Khawaarij, Raafidhwah, Baatwiniyyah na wakomunisti isipokuwa maangamivu na uharibifu duniani na Aakhirah.

Ni kweli kwamba ni lazima kuwanasihi watawala, lakini kwa mujibu wa Sunnah za kinabii na njia ya Salaf. Nasaha zinatakiwa kuwa za siri na kwa hekima. Kashfa na kuanikwa ni mambo hayakubaliwi na watu dhaifu, sembuse viongozi na watawala wake.

Tunamuomba Allaah atulinde kutokana na wapumbavu hawa. Ikiwa kuna kuangamia kwa ummah basi maangamivu hayo yatakuwa kupitia wao. Usalama, mwongozo na ukomavu ni katika maamrisho ya Allaah kisha maamrisho ya Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amekingwa na kukosea na mwenye kuwatakia watu kheri. Aliyajua yanayoufanya ummah wake kuwa mzuri na hivyo akawalingania kwayo. Aliyajua pia yanayoufanya ummah wake kuharibika na hivyo akawatahadharisha nayo.

Je, kuna ambaye anawatakia watu kheri, mkweli na mkweli katika nasaha zake kumshinda Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Je, kuna ambao wanawatakia watu kheri, wakweli na wakweli katika nasaha zao kuwashinda Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao waliishi wakati wa al-Hajjaaj alikuwa anamwaga damu lakini pamoja na hivyo wakawa wanawahimiza watu kufanya subira?

al-Hajjaaj na wengineo walikuwa wakimwaga damu na wakieneza ufisadi ardhini. Hata hivyo hakuna ambacho Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walichoamrisha isipokuwa kufanya subira. Wakati Madiynah walipomfanyia mapinduzi Yaziyd bin Mu´aawiyah Maswahabah walijitenga mbali nayo; Jaabir, Ibn ´Umar, Abu Sa´iyd al-Khudriy na wengineo (Radhiya Allaahu ´anhum).  Walikuwa wakiwatahadharisha watu kutokana na kuvunja kiapo na kumfanyia uasi kiongozi wao. Hawakufata upepo na wale walioingia katika fitina. Wafanya mapinduzi wakasahau maamrisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo kukatokea mtihani mkubwa ambao hautosahaulika. Baadhi ya hawa ambao wanachochea juu ya mimbari hakuna wanachotaka isipokuwa haya. Wengine masikini hawajui matokeo ya yale wanayosema. Hata hivyo wanapelekwa na hisia za upofu na wanafanya yale yanayotakwa na maadui. Natija ya mambo hayo inakuwa mbaya ya kuangamiza na mbaya sana. Yule ambaye anautakia ummah huu kheri basi ashikamane na mwongozo wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa, kila kilichozuliwa ni Bid´ah, kila Bid´ah ni upotofu na kila upotofu ni Motoni.

Allaah atulinde sisi, nyinyi na ummah kutokana na upotofu huu ambao unatoka kwa maadui wa Uislamu na unanasibishwa katika Uislamu kimakosa.

[1] Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ee ´Uthmaan! Allaah atakuvisha shati. Wanafiki wakikutana uivue basi usiivue mpaka utapokutana nami.” (Ahmad (6/75), at-Tirmidhiy (3715) aliyeisahihisha na Ibn Maajah (112). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwilaal-ul-Jannah” (1178-1179)

[2] al-Bukhaariy (3603) na Muslim (1843).

[3] al-Bukhaariy (7054).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kashf-us-Sitaar, uk. 37-40
  • Imechapishwa: 10/11/2022