Swali: Vipi kuhusu kuuza waqf?

Jibu: Ikiwa manufaa yake yameharibika basi huuzwa. Baadhi ya wanazuoni wamesema kwamba ikiwa kuuza kunaleta manufaa zaidi, basi inajuzu kwa upande wa kumfaidisha mwenye kuliweka kuwa waqf. Hivyo ikiwa upo katika eneo lisilofaa au mazao yake yamepungua kisha akaliuza kwa lile lililo bora zaidi, katika hali hiyo hakuna neno. Lakini maoni yaliyotangaa kwa wanazuoni ni kwamba ikiwa manufaa yake yameharibika au yanakaribia kuharibika, kama katika maeneo ambayo watu wake wamehama na nyumba haifai kitu tena, kodi yake ni ndogo, basi huuzwa na kutafutwa nyumba nyingine katika eneo linalotakiwa.

Swali: Ikiwa aliweka jengo kuwa waqf akasema kodi yake ni yenu lakini nikifa na wakihitaji watoto wangu waichukue?

Jibu: Hiyo si waqf. Huko ni kutoa tu faida ya kodi.

Swali: Vitabu vinahesabiwa kuwa ni katika elimu?

Jibu: Ndio, kuviweka vitabu kuwa waqf ni katika elimu.

Swali: Lakini kavifanya waqf nyumbani kwake kwa ajili ya nyumba yake?

Jibu: Haitwi waqf isipokuwa akiviweka kuwa waqf. Ama akiviweka kwa warithi wake – kwa watoto wake kama urithi – haitwi waqf, lakini watu wakifaidika navyo basi kunatarajiwa juu yake kheri.

Swali: Vipi ikiwa ameweka mali yake yote kuwa waqf?

Jibu: Ikiwa yuko mzima basi bora ajiwekee baadhi ya mali yake, kama Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyomwambia Ka´b bin Maalik:

”Shikilia baadhi ya mali yako.”

Maana yake ni kwamba jiwekee kitu kinachokuendesha maisha yako na weka kuwa waqf kile kinachowezekana ili asije kuhitaji na kuwa masikini anayeomba watu. Kwa hiyo ajiwekee baadhi ya mali yake.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/25411/ما-ضوابط-الوقف-وهل-يجوز-بيعه
  • Imechapishwa: 23/12/2025