Swali: Siku ya ´iyd ikikutana na siku ya ijumaa swalah ya ´iyd inatosheleza kutokamana na siku ya ijumaa? Mtu akiswali siku ya ijumaa swalah yake inazingatiwa ni kafara mpaka ijumaa ya kufuata?

Jibu: Siku ya ´iyd ikikutana na siku ya ijumaa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebainisha kuwa swalah ya ´iyd inatosheleza kutokamana na swalah ya ijumaa na badala yake watu wataiswali kwa aina ya Dhuhr. Hapa ni pale ambapo mtu akiswali pamoja na wengine swalah ya ´iyd. Maimamu misikitini wataswalisha swalah ya ijumaa na wawaswalishe wahudhuriaji. Ambaye hatohudhuria swalah ya ´iyd basi aswali nyumbani au pamoja na ndugu zake kwake Dhuhr. Hivo ndivo alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Allaah ameijaalia ijumaa kuwa ni kafara na kifutio endapo mtu atajitwahirisha nyumbani kwake ambapo akaja na kuswali kiasi ambacho Allaah amemwandikia, akanyamaza na kusikiliza Khutbah, asipenyeze kati ya watu wawili na asimuudhi yeyote, basi swalah ya ijumaa inakuwa kafara na kifutio kwa yale yaliyoko baina yake na ijumaa nyingine ukiongezea masiku matatu. Kusema kwamba ni kifutio au kafara haina maana kwamba inadondosha vipindi vyengine vya swalah vilivyo baada yake na haki nyenginezo mbalimbali. Sivyo hivyo. Bado anatakiwa kutekeleza haki zinazomuwajibikia, amche Allaah na atekeleze haki mbalimbali katika nyakati zote. Ni mamoja haki hizo ni swalah au nyenginezo. Ni lazima awe na mapungufu. Kwa hivyo swalah ya ijumaa hii inakuwa ni kafara na kifutio cha madhambi madogomadogo anayoweza kufanya.

Kuhusu mambo ya wajibu bado ni lazima kwake kuyatekeleza. Baadhi ya wajinga wanadhani kwamba swalah ya ijumaa inawatosheleza na hivyo wanaacha vipindi vyengine vya swalah. Hii ni dhambi kubwa, ukafiri na upotevu. Kusema kwamba ijumaa ni kafara na kifutio ni kama mfano wa tawbah na vipindi vitano vya swalah pia ni kafara na kifutio. Hata hivyo haina maana kwamba mtu ambaye anaswali ijumaa aharibu swalah nyenginezo na kufikiri kwamba kafara na kifutio kinamtosheleza mpaka ijumaa nyingine ambapo akapoteza haki mbalimbali zengine na haamrishi mema, hakatazi maovu, anakuwa na utovu wa nidhamu kwa wazazi wawili, akawakata ndugu zake, akashuhudia uongo na akaleta madai ya batili na huku anakusudia kwamba ijumaa aliyoswali inamtosheleza. Sivyo hivyo. Huo ni ujinga mkubwa na upotofu wa mbali kabisa.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/2621/%D8%A7%D8%AC%D8%B2%D8%A7%D8%A1-%D8%B5%D9%84%D8%A7%D8%A9-%D8%A7%D9%84%D8%B9%D9%8A%D8%AF-%D8%B9%D9%86-%D8%A7%D9%84%D8%AC%D9%85%D8%B9%D8%A9-%D9%88%D8%B5%D9%84%D8%A7%D8%AA%D9%87%D8%A7-%D8%B8%D9%87%D8%B1%D8%A7
  • Imechapishwa: 30/07/2020