“Kuna tofauti katika mambo haya” – ima mjinga au kitu linalofuata matamanio

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Hii ni njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni na wala msifuate njia za vichocoro zikaja kukufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo alivyokuusieni kwayo mpate kuwa na uchaji.” (06:153)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wale wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni njia bora na matokeo mazuri zaidi.” (04:59)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika yule atakayeishi kipindi kirefu katika nyinyi basi ataona tofauti nyingi. Hivyo basi, jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego yenu… ”

Hivi ndivyo anavyotuamrisha Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba wakati wanachuoni wanapotofautiana katika masuala fulani, basi tuchukue kutoka katika maoni yao yale ambayo ni yenye kuafikiana na Qur-aan na Sunnah na kuacha yale yenye kwenda kinyume na dalili. Hii ndio alama ya kumuamini Allaah na siku ya Mwisho na kwamba ni bora kwetu na mwisho mwema. Vilevile amesema ya kwamba iwapo tutachukua yale maoni yanayoenda kinyume na dalili, basi yatatutenganisha na Njia ya Allaah na hatimaye kututumbukiza katika njia ambayo ni ya upotevu. Hivyo ndivyo alivyoeleza kuhusu mayahudi na manaswara ya kwamba wamewafanya wanazuoni wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Allaah. Pindi ´Adiyy bin Haatim (Radhiya Allaahu ´anh) alipotatizika ni vipi walikuwa wakiwafanya kuwa ni waungu wao badala ya Allaah ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akambainishia kuwafanya waungu badala ya Allaah ya kwamba ni kule kuwatii katika kuhalalisha yale aliyoharamisha Allaah na kuharamisha yale aliyohalalisha Allaah.

Watu wengi hii leo unapowaona wanaenda kinyume na ukawakataza utawasikia wanakwambia:

“Kuna tofauti katika mambo haya.”

Anatumia jina la “tofauti” kama hoja kwa yale aliyomo hata kama yatakuwa ni yenye kwenda kinyume na dalili. Ni ipi tofauti kati yake na yale waliyokuwemo mayahudi na manaswara ambao walikuwa wakiwafanya wanazuoni wao na watawa wao kuwa ni waugu badala ya Allaah?

Lililo la wajibu juu ya watu hawa ni kumcha Allaah na watambue kuwa kuwepo tofauti juu ya mambo fulani hakuwajuzishii kwenda kinyume na dalili. Hali imefikia kiasi cha kwamba wajinga wengi wanatafuta maoni mbali mbali yaliyorekodiwa kwenye kompyuta yaliyonukuliwa kutoka katika vitabu vilivyo na maoni mbali mbali. Matokeo yake anafuata lile jibu linaloafikiana na matamanio yake kutoka katika yale maoni mbali mbali pasi na kupambanua kati ya yale yaliyosimama juu ya dalili sahihi na yale ambayo ni kinyume na hivyo. Mtu huyu anafanya hivo ima kwa sababu ya ujinga wake au kwa sababu ya kufuata matamanio yake moyoni. Haijuzu kwa mjinga kuzungumza juu ya Shari´ah ya Allaah kujengea yale aliyosoma au kuyasikia katika mkanda uliyorekodiwa ilihali hajui usahihi wake au mashiko yake kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Allaah hakutuamrisha kurejea katika yale yaliyomo katika vitabu vya wanachuoni pasi na mtu kufahamu kitu. Kinyume chake ametuamrisha kuwauliza wanachuoni. Amesema (Subhaanah):

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

“Basi waulizeni watu wenye Ukumbusho ikiwa hamjui.” (16:43)

Haijuzu kwa mtu anayefuata matamanio kuyafanya matamanio yake kuwa mungu badala ya Allaah kwa njia ya kwamba anachukua kutoka katika maoni mbali mbali yale yanayoafikiana na matamanio yake na kuacha yale yasiyoafikiana na matamanio yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّنِ اتَّبَعَ هَوَاهُ بِغَيْرِ هُدًى مِّنَ اللَّـهِ

“Ni nani mpotofu zaidi kuliko yule aliyefuata matamanio yake pasi na mwongozo kutoka kwa Allaah?” (28:50)

أَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ أَفَأَنتَ تَكُونُ عَلَيْهِ وَكِيلًا

“Je, umemuona yule aliyefanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Je, hivi wewe utaweza kuwa ni mdhamini wake?” (25:43)

Haijuzu kwa yule mwenye elimu akawapekulia watu yale yanayoafikiana na matamanio yao asije akawapoteza kutokamana na njia ya Allah kwa kutumia hoja ya kuwepesisha mambo. Wepesi unakuwa katika kufuata dalili. Kunakhofiwa mtu huyu asije kuingia katika wale ambao Allaah amesema kuwahusu:

لِيَحْمِلُوا أَوْزَارَهُمْ كَامِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۙ وَمِنْ أَوْزَارِ الَّذِينَ يُضِلُّونَهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ

“… ili wabebe madhambi yao kamili siku ya Qiyaamah na madhambi ya wale waliowapoteza bila ya elimu.” (16:25)

Allaah awawafikishe wote katika elimu yenye manufaa na matendo mema.

Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

Imeandikwa na:

Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan

Mwanachama wa baraza la Kibaar-ul-´Ulamaa’.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://alfawzan.af.org.sa/node/13194
  • Imechapishwa: 29/01/2017