Kumtuma mnyama wa ´Aqiyqah na Udhhiyah nje ya nchi

Swali: Baadhi ya watu wanatuma vichinjwa vya Udhhiyah au ´Aqiyqah katika baadhi ya nchi kupitia njia za watu au thamani yake na hivyo wanaenda kinyume na Sunnah ya kinabii. Ni yapi maelezo yako juu ya hilo?

Jibu: Bora ni kuchinja ´Aqiyqah nyumbani kwako. Kichinjwa cha ´Aqiyqah ni baada ya kuzaa mtoto mchanga. Ni kondoo au mbuzi wawili kwa ajili ya mtoto wa kiume na kondoo au mbuzi mmoja kwa ajili ya mtoto wa kike. Hiyo ndio inaitwa ´Aqiyqah na baadhi ya watu wanaita kuwa ni Tamiymah au Nusaykah. Ni Sunnah iliyokokotezwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kumchinjia mtoto wa kiume kondoo au mbuzi wawili na mtoto wa kike kondoo au mbuzi mmoja. Anachinjwa siku ya saba. Hivo ndio bora. Mtu amchinje nyumbani kwake siku ya saba na ale sehemu yake na awalishe awatakao katika majirani zake, jamaa zake na wengineo. Au amgawanye na amtoe swadaqah na asimgawanye nchi za nje. Bora amgawanye nyumbani kwake na ale sehemu yake na sehemu nyingine awalishe wengine.

Hapana neno pia akimtuma nje ya nchi kwenda kwa wapambana jihaad au wengineo kupitia mawakala wenye kuaminika ambao watawachinja huko na kuwagawanya. Hata hivyo bora na Sunnah ni kule kumchinja nyumbani kwake na baina ya familia yake na wahuishe na kudhihirisha Sunnah kati yao na majirani zake na wamle wao na wawalishe wengine.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/21237/حكم-ارسال-الاضحية-او-العقيقة-خارج-بلدها
  • Imechapishwa: 09/06/2024