Kumtenga imamu anayeswali zaidi ya Rak´ah kumi na moja

Swali: Kuna ambao wanaswali na imamu Rak´ah kumi na moja halafu wanatengana naye kwa hoja ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hazidishi si Ramadhaan wala mwezi mwingine Rak´ah kumi na moja.

Jibu: Kitendo hichi ambacho ni kutengana na imamu ambaye anaswali Tarawiyh zaidi ya Rak´ah kumi na moja kinaenda kinyume na Sunnah na kujinyima ule ujira na thawabu zinazotarajiwa. Isitoshe ni kwenda kinyume na yale waliyokuwemo as-Salaf as-Swaalih. Waliokuwa wakiswali pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa hawamwachi kabla yake. Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakiafiana na maimamu wao japokuwa amezidisha katika yale wanayoonelea wao kuwa ndio yaliyowekwa katika Shari´ah. ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) aliposwali kikamilifu Minaa walimkemea lakini hata hivyo walikuwa wakimfuata katika kukamilisha na wakisema:

“Hakika tofauti ni shari.”

Vilevile ni kujikoseshea zile thawabu zinazopatikana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza basi anaandikiwa kuwa ameswali usiku mzima.”

Kuzidisha juu ya Rak´ah kumi na moja sio haramu. Bali ni katika mambo yanayojuzu. Dalili ya hilo ni kuwa kuna mtu alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu swalah ya usiku ambapo akasema:

“Ni mbili mbili. Atapochelea mmoja wenu kuingia kwa asubuhi basi aswali moja ili kuwitirisha aliyoswali.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuwekea mpaka ya idadi maalum. Lau ingelikuwa kuzidisha zaidi ya Rak´ah kumi na moja ni haramu basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angelibainisha hilo.

Kwa hivyo ninawanasihi ndugu zangu wamfuate imamu mpaka atapomaliza.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (14/205-206)
  • Imechapishwa: 17/06/2017