Swali: Je, inafaa kumtembelea mgonjwa ndugu ambaye ni kafiri?

Jibu: Anatembelewa hata kama ni kafiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtembelea Abu Twaalib hali ya kuwa ni kafiri. Isitoshe alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mtumishi wa kiyahudi huko Madiynah. Siku moja akawa mgonjwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtembelea na akamwambia:

”Shuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba mimi ni Mtume wa Allaah.” Kijana huyo alikuwa na baba yake ambaye alimwambia: ”Mtiini Abu al-Qaasim.” Hatimaye kijana yule akasema: ”Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatoka pale hali ya kuwa ni mwenye kusema:

”Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye amemuokoa na Moto kupitia kwangu.”

Alikuwa ni mfanyakazi kabla ya makafiri kuamrishwa kutolewa katika Bara Arabu. Kwa hivyo akamtembelea hali ya kuwa ni myahudi na vilevile akamtembelea Abu Twaalib hali ya kuwa ni mshirikina na khaswa ikiwa matembezi hayo yanatarajiwa kheri ya kumlingania kwa Allaah. Pengine kwa kufanya hivo Allaah akamuokoa kupitia kwake.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/24449/حكم-عيادة-المريض-الكافر
  • Imechapishwa: 12/10/2024