Swali: Kuna siku moja ya Ramadhaan ambayo nilikuwa msafiri sikufunga mpaka nikafikiwa na Ramadhaan ya pili na sikulipa siku hii ambayo ilinipita. Je, inajuzu kwangu baadaye kuilipa kwa sababu mwaka umeshapita na sikulipa?

Jibu: Ni jambo linalotambulika kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Mtu huyu alikuwa msafiri na akala siku moja basi ni lazima kwake kuilipa kwa ajili ya kutekeleza amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni lazima vilevile ailipe ndani ya mwaka wake. Kwa msemo mwingine haifai kuichelewesha mpaka kukaingia Ramadhaan ya pili. Hayo ni kutokana na maneno yake ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Nilikuwa nadaiwa swawm ya Ramadhaan na nashindwa kulipa mpaka katika Sha´baan. Hayo ni kutokana na nafasi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwangu.”

Maneno yake aliposema:

“… nashindwa kulipa mpaka katika Sha´baan.”

inafahamisha kwamba ni lazima kulipa kabla ya kuingia Ramadhaan ya pili. Lakini akichelewesha mpaka akaingiliwa na Ramadhaan ya pili basi ni lazima kwake kumtaka Allaah msamaha, atubie Kwake, ajutie alichokufanya na alipe siku hii. Kwa sababu ulipaji haupotei kwa kuchelewesha. Hivyo ailipe siku hii na inamtosheleza. Kwa kufanya hivo itatakasika dhimma yake.

[1] 02:184-185

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (18) http://binothaimeen.net/content/6823
  • Imechapishwa: 25/03/2021