Swali: Licha ya kwamba tunahitajia kulingania kwa Allaah tumeshughulishwa na wale waliopewa mtihani wa kuingiwa na majini. Je, inafaa kuweka kando ulingano kwa ajili ya kufanya matabano? Inakuwa kumfanyia matabano aliyepatwa na jini? Je, ni sharti mtu achukue malipo?

Jibu: Kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall) ni faradhi kwa baadhi ya watu. Ikiwa kazi hiyo inasimamiwa na watu wenye kutosheleza basi kwa wengine inakuwa ni jambo linalopendeza. Ikiwa inamlazimu mtu kwa njia ya kwamba hakuna mwingine awezaye kusimama mahali pake, basi atatanguliza mbele jambo hilo juu ya kuwafanyia matabano wale waliopatwa na jini. Kwa sababu manufaa ya ulingano ni manufaa yenye uhakika tofauti na matabano ambayo manufaa yake ambayo si yenye uhakika. Ni watu wangapi waliosomewa lakin hawanufaiki kitu! Kwa ajili hiyo mtu anatakiwa kuzingatia hali ya mtu; ikiwa inamlazimu kulingania kwa namna ya kwamba hakuna mwingine awezaye kusimama mahali pake, basi atalazimika kulingania ingawa itapelekea kuacha kuwafanyia matabano wale walioingiwa na majini. Ama ikiwa haimlazimu, atatazama ni kipi chenye manufaa zaidi. Ikiwa anaweza kukusanya kati ya hayo mawili, jambo ambalo ndio udhahiri kwamba anaweza kukusanya kati ya hayo mawili, basi atatenga masiku juu ya kila kimoja katika hivyo viwili kutegemea na umuhimu. Namna hiyo anakuwa anawatendea wema wale ndugu zake ambao wamesibiwa na msiba huu na sambamba na hilo anaendelea kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall). Akiweza kukusanya kati ya hayo mawili ndio bora zaidi.

Kuhusu matibabu sahihi kwa yule aliyepatwa na jini, inatofautiana kutegema na hali. Lakini bora ni yeye kumsomea Qur-aan ikiwa ni pamoja na:

يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ إِنِ اسْتَطَعْتُمْ أَن تَنفُذُوا مِنْ أَقْطَارِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ فَانفُذُوا ۚ لَا تَنفُذُونَ إِلَّا بِسُلْطَانٍ فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ يُرْسَلُ عَلَيْكُمَا شُوَاظٌ مِّن نَّارٍ وَنُحَاسٌ فَلَا تَنتَصِرَانِ فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ

“Enyi jamii ya majini na wanadamu! Mkiweza kupenya kwenye mbingu na ardhi, basi penyeni. Hamtoweza kupenya isipokuwa kwa mamlaka. Basi ni zipi katika neema za Mola wenu mnazikadhibisha? Mtapelekewa muwako wa moto juu yenu na shaba iliyoyayushwa, basi hamtoweza kujinusuru. Basi ni zipi katika neema za Mola wenu mnazikadhibisha?”[1]

Hapa wanatiliwa mkazo ya kwamba hawawezi kumkimbia Allaah (´Azza wa Jall). Vilevile mtu anatakiwa kumsomea ”al-Falaq”, ”an-Naas”, ”al-Ikhlaasw” na Aayah al-Kursiy yule aliyeingiwa na jini. Aidha awape mawaidha na kuwakataza majini hao kuwaudhi waislamu, kama alivyokuwa akifanya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah).

Kuhusu kupokea malipo, bora ni yeye kutofanya hivo. Akichukua malipo bila ya shari hapana vibaya. Ikiwa hawa walipatwa na majini wamepuuzia haki ya mfanya matabano ambapo mfanya matabano akakataa kuwafanyia matabano isipokuwa mpaka wamlipe, hapana vibaya. Hayo yanafahamishwa na Hadiyth ya Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kuna kikosi cha Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kilikuwa katika safari wakati walipotua kwenye kabila la mwarabu mmoja. Wakaomba wapokelewe kama wageni, lakini wakakataa. Mkuu wa kabila lile akawa amedungwa na nyoka. Wakajaribu kumtibu kwa kila njia, lakini haikusaidia kitu. Baadhi yao wakasema: “Nendeni kwa lile kundi lililokuja. Huenda wana kitu.” Wakaenda na kusema: “Mkuu wetu amedungwa na nyoka. Tumejaribu kumtibu kwa kila njia, lakini haikusaidia kitu. Je, kuna yeyote katika nyinyi ana chochote?” Mmoja wao akasema: “Ninaapa kwa Allaah ya kwamba nina tiba, lakini ninaapa kwa Allaah ya kwamba tumewaomba mtupokee kama wageni, lakini mmkakataa. Sintowatibu mpaka mtupe ujira kwa hilo.” Wakakubaliana kundi kadhaa la kondoo. Akaanza kumtemea cheche za mate na kusoma:

الْحَمْدُ للّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Himdi zote njema ni Zake Allaah, Mola wa walimwengu.”[2]

Mtu yule akapata uchangamfu kana kwamba ameachwa huru kutokana na hatamu. Akaanza kutembea na kutohisi maumivu yoyote. Wakawapa ujira ambao walikubaliana. Baadhi yao wakasema: “Agawanywe.” Wengine wakasema: “Msifanye chochote mpaka tufike kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza yaliyopitika, tuangalie atatuamrisha nini.” Wakafika kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza yaliyopitika. Akasema: “Umejuaje kuwa [Suurah hii] inatibu?” Kisha akasema: “Mmefanya jambo la sawa. Mgaweni na mnipe sehemu” na akaanza kucheka.”[3]

[1] 55:33-36

[2] 01:01

[3] al-Bukhaariy (2276) na Muslim (2201).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/33-35)
  • Imechapishwa: 07/07/2026