Swali:

السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

Katika baadhi ya miji tunaona watu wakibusiana wakati wa kufanyiana tanzia. Kwa kuzingatia kwamba kupeana pole misibani ni Sunnah inayotokana na dalili, nimejaribu kutafuta dalili ya kushumiana wakati wa kupeana pole. Hata hivyo sikupata dalili yoyote wala maoni juu ya kitu hicho. Kitu pekee nilichopata ni kwamba Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) ametaja katika kitabu chake “al-Mughniy” kwamba Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ukitaka, utashika mkono wa yule aliyefikwa na msiba wakati wa kumpa pole, na ukitaka hutofanya hivo.”

Dr az-Zuhayliy amesema katika “Fiqh-ul-Islaam wa Addillatuh”:

“Haikuchukizwa kuamkuana kwa kupeana mikono na yule ambaye amefikwa na msiba au kumshika mkono.”

Shaykh al-Albaaniy ambaye ni kigogo katika Hadiyth na elimu zake hakututajia katika kitabu chake “Ahkaam-ul-Janaa-iz” chochote muhimu kuhusiana na mada hii. Bali nilichofahamu kutoka katika kitabu chake “Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah” ni kwamba kubusiana hakukuwekwa katika Shari´ah isipokuwa kwa yale ambayo yamefahamishwa na dalili, kama kumbusu aliyefika kutoka safarini, kuwabusu watoto na wanandoa na mfano wa hayo ambayo yamethibiti katika Sunnah. Nilikuwa napenda utoe maoni yako juu ya suala hili.

Jibu:

بسم الله الرحمن الرحيم

و عليكم السلام و رحمة الله و بركاته

Mambo ni kama ulivosema si Sunnah kubusiana wakati wa tanzia. Wala haikupokelewa kutoka kwa yeyote katika Salaf. Kwa hivyo kuliacha ndio Sunnah na lililo salama zaidi, khaswa ikiwa inapelekea kumkera yule aliyefikwa na msiba. Aidha busu muda unavokwenda busu hizi zinaweza kupea. Tunamuomba Allaah atuongoze sisi na ndugu zetu katika yale anayoyaridhia.

Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

1413-03-28

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/355-356)
  • Imechapishwa: 14/05/2021