Kuandika ”Allaah” ”Muhammad” ukutani

Swali: Hili swali limeleta mzozo kwa watu wengi. Kulikuwa kumeandikwa neno ”Allaah” na ”Muhammad” kwa njia ya maneno hayo mawili kuingiliana juu ya mlango wa msikiti. Kuna ambao walisema kuwa haijuzu kuandika kwa sura kama hii na hoja yao ya kusema hivo ni kwamba kwa kuandika hivo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakuwa amefanywa katika ngazi ya Allaah, jambo ambalo haliingii akilini. Wengine wakasema kuwa kuandika hivo hakuna uharamu wowote kwa kuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) amefanya Jina Lake kuwa pembezoni mwa Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tunaomba kutoka kwenu mwelekezo sahihi.

Jibu: Miongoni mwa mambo yaliyokuja katika Shari´ah kushuhudia kati ya upwekekaji wa Allaah na kushuhudia ujumbe kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mambo yenye kwenda sambamba katika baadhi ya sehemu ikiwa ni pamoja na adhaana na Iqaamah. Vilevile katika Hadiyth ifuatayo:

”Uislamu umejengwa juu ya [mambo] matano; kushuhudia ya kwamba hakuna mungu mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah…”

Na mambo mengine pamoja na kubainisha ambayo ni wajibu kwa mja kuyaamini kwa nisba ya shahaadah hizo mbili kulingana na yale ambayo kila mmoja anastahiki kama mfano wa kauli ya mja ”nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.”

Ama kuhusiana na kuyaandika hayo kwa kuyachanganya hakukuthibiti kitu kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Mbali na hilo ni kwamba jambo hilo lina khatari kubwa kwa sababu linafanana na ´Aqiydah ya manaswara ya utatu na kwamba baba, mwana na roho mtakatifu wote ni mungu mmoja. Isitoshe jambo hilo linaashiria ´Aqiydah ambayo ni batili, nayo ni ´Aqiydah ya Wahdat-ul-Wujuud. Jengine ni kwamba jambo hilo linapelekea katika kuvuka mipaka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuabudu pamoja na Allaah (Subhhaanah).

Kujengea juu ya haya ni wajibu kukataza kuandika Jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na jina la Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sura kama hii ya kuandika maneno hayo mawili yakaingiliana, herufi za neno hili zikaingia kwenye neno lingine. Bali haijuzu hata kuandika ”Allaah” ”Muhammad” kwenye mlango wa msikiti wala mlango mwingine kutokana na utatizi tuliotaja na mengineyo.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (01/40)
  • Imechapishwa: 06/10/2020