Kuamini kuwa siku fulani ina mkosi na kwamba ni siku nyeusi

Swali: Baadhi ya watu wanapopatwa na ajali katika siku ya jumamosi, kwa mfano, husema kwamba  jumamosi hiyo ni nyeusi au kwamba ni siku yenye nuksi. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Asiseme hivyo, kwani jumamosi wala jumapili hazina chochote cha kipekee. Ni kweli Allaah ametaja kuhusu watu wa ´Aad kuwa walipatwa na adhabu katika “siku zenye nuksi”, kama Allaah alivyosema:

فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي أَيَّامٍ نَّحِسَاتٍ

”Tukawapelekea upepo wa kimbunga katika siku za mikosi.”[1]

Kwa hiyo mtu akisema kuwa siku aliyopatwa na ajali ni “siku ya nuksi” au “siku yenye kuchukiza”, basi ni kwake yeye binafsi na si kwa asili ya siku hiyo, kama ilivyokuwa kwa watu wa ´Aad.

Swali: Baadhi ya ndugu walioko ughaibuni huambiana “Siku yako ni nyeusi.” Unasemaje kuhusu hili?

Jibu: Haifai kusema maneno kama haya. Inafaa amfariji ndugu yake na kumwambia “Subiri ewe ndugu yangu na utarajie thawabu kutoka kwa Allaah.” Asiongeze huzuni juu ya huzuni. Aseme naye kwa maneno ya kutuliza moyo “Mambo yote yako mikononi mwa Allaah na mtu hupewa ujira kwa msiba wake.” Kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ajabu iliyoje juu ya jambo la muumini. Hakika mambo yake yote huwa ni kheri. Na hilo haliwi kwa mwingine isipokuwa tu muumini. Akifikwa na kitu cha kufurahisha basi hushukuru na ikawa ni kheri kwake. Na akifikwa na kitu cha kusononesha basi husubiri na ikawa ni kheri kwake.”[2]

Kwa hiyo asiseme “Siku nyeusi” au “siku mbaya” au “wewe huna kheri.” Bali aseme “Subiri ewe ndugu yangu, mambo yako mikononi mwa Allaah na subira yako ni kwa msaada wa Allaah. Sema:

إنا لله وإنا إليه راجعون

”Hakika sisi ni wa Allaah na hakika Kwake ndiko kutarejea.”

na maneno mazuri kama hayo.

[1] 41:16

[2] Muslim (2999) na Ahmad (4/332).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/31238/ما-حكم-التشاوم-بيوم-السبت-ووصفه-بالاسود
  • Imechapishwa: 15/10/2025