Kinachosimangwa kwa wafuasi wa madhehebu

Swali: Kuna tofauti gani kati ya madhehebu manne? Je, kuna madhehebu bora kuliko mengine?

Jibu: Madhehebu manne yote yanatafuta haki. ash-Shaafi´iyyah, Maalikiyyah, Hanbaliyyah na Hanafiyyah yote ni madhehebu yaliyolenga kufuata haki. Wote walifuata Qur-aan na Sunnah. Allaah awarehemu na awaridhie. Lakini lawama ipo kwa baadhi ya wafuasi wao kwa kufata kibubusa na kung’ang’ania misimamo ya madhehebu yao.

Kuna pia madhehebu ya Dhwaahiriyyah ambayo ni madhehebu ya tano yanayojulikana. Pia yalikuwepo madhehebu mengine yaliyopita kama vile al-Jariyriyyah, al-Laythiyyah, ath-Thawriyyah; wafuasi wa Sufyaan ath-Thawriy, wafuasi wa al-Layth bin Sa‘d, wafuasi wa Ibn Jariyr na ar-Raahawiyyah ambao ni wafuasi wa Ishaaq bin Raahawayh. Lakini haya yamepotea.

Kilicho muhimu ni kufuata haki. Haya madhehebu manne, pamoja na Dhwaahiriyyah na yaliyotangulia kabla ya hayo yaliyopotea, yote yalikuwa na lengo la kufuata haki. Huenda wakatofautiana katika suala moja, mawili au matatu, na ikawa ndio masuala yaliyomfanya mwanachuoni fulani ajulikane. Kisha akawa ana wafuasi wanaofuata maoni hayo. Hapo mwelekeo huo ukajulikana kama madhehebu maalum. Tofauti hizi mara nyingi ni katika masuala madogo ya matawi yasiyoathiri misingi ya dini. Lakini lawama ipo kwa mtu kufanya chuki au kufuata kibubusa na kuendelea kushikilia mambo yasiyo sahihi na kukataa haki miongoni mwa wafuasi. Hilo ndilo linalosimangwa. Ama madhehebu yote yanatambulika kuwa yanataka haki, kufuata Qur-aan na Sunnah na yanakusudia kufuata kile alichokuja nacho Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/979/الفرق-بين-المذاهب-الاربعة
  • Imechapishwa: 29/12/2025