Kila mmoja anaifasiri Qur-aan kwa mujibu wa elimu aliyopewa na Allaah

Swali: Ikiwa wanazuoni wa Uislamu wa mwanzo na wa zama hizi hawakuweza kuizingira elimu ya tafsiri ya Qur-aan kwa ukamilifu, basi vipi wanaweza kuitafsiri au kuitafsiri kwa lugha zisizo za Kiarabu?

Jibu: Wanatafsiri kile kilichowabainikia. Hakuna yeyote anayeweza kusema kwamba ameizingira kwa elimu yote yaliyomo ndani ya Kitabu cha Allaah. Kinachofanyika ni kwamba mtu anatafsiri kile Allaah alichomrahisishia kukielewa. Juu ya kila mwenye elimu yupo mwenye elimu zaidi. Kwa hiyo kila mfasiri na kila mtafsiri hufanya tafsiri kulingana na kiwango cha elimu ambacho Allaah amempa. Ikiwa ana elimu, anajitahidi na anamcha Allaah, basi anatafsiri na kufasiri kwa kadiri ya uwezo wake. Haipasi kutokana na hilo kudai kwamba lazima awe ameizingira Qur-aan kwa elimu yote. Wala haipasi kwa sababu hiyo kuzuiwa tafsiri au ufafanuzi. Kila mmoja hufanya kwa mujibu wa elimu aliyopewa na Allaah. Lau ingesemwa kwamba hapaswi kutafsiri, wala kufasiri na wala kuzungumza isipokuwa yule aliyeizingira Qur-aan na Sunnah kwa elimu yote, basi hakuna mtu yeyote ambaye angepata manufaa.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1619/حكم-ترجمة-معاني-القران-مع-عدم-الاحاطة-بتفسير-القران
  • Imechapishwa: 28/06/2026