Kijana anataka kuoa lakini hayuko tayari kupokea michango ya watu

Swali: Mimi ni kijana ninayesumbuliwa na matamanio kwa njia ya kwamba baadhi ya nyakati yananizidi na wakati mwingine mimi nayazidi na nachelea nisije kutumbukia katika maasi yanayoharibu moyo na dini. Nataka kuoa lakini sina mali. Kuna mtu anayetaka kunipa pesa ili nioe. Lakini hata hivyo nafsi yangu inakataa kuchukua pesa kutoka kwa mwingine. Ni kitu gani kinachopendwa zaidi na Allaah; kupokea pesa hiyo au nijichunge na machafu mpaka pale Allaah ataponitajirisha kutoka katika fadhilah Zake? Namuomba Allaah akupende kama ninavyokupenda mimi kwa ajili Yake.

Jibu: Allaah akujaze kheri. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلْيَسْتَعْفِفِ الَّذِينَ لَا يَجِدُونَ نِكَاحًا

“Wajizuilie na machafu wale ambao hawapati uwezo wa ndoa… “

Mpaka lini?

حَتَّىٰ يُغْنِيَهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ

”… mpaka Allaah awatajirishe katika fadhilah Zake.”[1]

Lakini ni vipi Allaah anamtajirisha mja Wake kutoka katika fadhilah Zake? Je, unafikiri kuwa atakuteremshia kutoka mbinguni dhahabu na fedha? Hapana. Bali maana yake ni kwamba mpaka pale Allaah atapomfanyia wepesi wa utajiri kwa njia yoyote iliyoruhusiwa. Ni mamoja kwa kurithi, kupewa zawadi, kuchuma au njia nyenginezo. Kwa sababu Allaah hakubainisha ni kwa njia gani mtu atapata utajiri huo.

Hivyo namwambia midhali pesa imekujia kutoka kwa mwingine na wakati huohuo wewe hukuiomba basi ipokee na uoe kwayo. Namuomba Allaah akubariki kwa kuoa kwako. Ikiwa anaoa siku za usoni, basi atualike kwenye karamu yake ya ndoa – Allaah akitaka.

[1] 24:33

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (55) http://binothaimeen.net/content/1250
  • Imechapishwa: 28/06/2020