Kazi za uwakili hii leo kwa mtazamo wa al-Albaaniy

Swali: Ni ipi hukumu ya kufanya kazi katika korti au katika makampuli ya mawakili katika nchi inayohukumu kwa sheria zilizotungwa na wanadamu zenye kutoka magharibi na sio kwa Shari´ah?

Jibu: Sionelei kufaa kufanya kazi ya uwakili hii leo kutokana na sababu iliyotajwa na ndugu muulizaji. Isipokuwa ikiwa kama tutakadiria hali ambayo ni nzito sana ambayo nafikiri kuwa haiwezi kutekelezwa na yeyote isipokuwa yule ambaye amepambika kwa sifa mbili tukufu hii leo:

1- Wakili awe amesoma elimu ya Shari´ah iliyojengeka juu ya Qur-aan na Sunnah kama ambavo amesoma kanuni za kilimwengu. Hili peke yake linakaribia kuwa jambo ni jambo lisiloweza kupatikana. Mawakili hawa ambao husoma kanuni za kilimwengu hutumia miaka mingi katika jambo hilo. Ni wakati gani ataweka muda wake wa kusoma Shari´ah ya Kiislamu iliyojengeka juu ya Qur-aan na Sunnah? Ni kama ambavo ni lazima kwa kila mwanachuoni anayetaka kuchukua hukumu ya ki-Shari´ah.

2-  Wakili anatakiwa kuwa na uchaji wa hali ya juu. Wakati anapomjia mteja na kumtaka atetee haki yake, basi anatakiwa kudurusu haki yake kwa mujibu wa zile elimu mbili alizonazo; Qur-aan na Sunnah na kanuni alizosomea. Akipata njia inayoweza kumpa mteja haki yake kwa njia ya kikanuni na wakati huohuo haipingani na Shari´ah, basi amtetee. Kwa mtazamo wangu naona kwamba ikiwa wakili ataweza kufanya hivo ni kwa mwaka mmoja au miwili peke yake. Baadaye kwa haraka sana nafsi huvutiwa katika matamanio na akaacha kutafuta haki, pasi na kujali inamuhusu yule mteja wake au yeye mwenyewe. Baadaye hufuata maslahi ya kipesa.

Hili ni jambo gumu sana. Kwa ajili hiyo nasema kwamba haijuzu kufanya kazi ya uwakili iliyojengeka juu ya sheria zilizotungwa na wanadamu hii leo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Juddah (20 B)
  • Imechapishwa: 07/12/2020