Swali: Baadhi ya Da´wah ambazo hazilingaii katika Tawhiyd ni sababu ya kutahadharisha kutokamana nao? Wanasema kuwa wako katika maeneo ambayo hakuna shirki na kwamba hivyo wametoshelezwa na jambo hilo.

Jibu: Tawhiyd ndio msingi wa misingi na ndio msingi wa mila na msingi wa dini ya Allaah. Msingi huo umetajwa na Allaah:

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ

 “Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.” (47:19)

Mlinganizi ambaye analingania katika dini ya Allaah ni lazima akumbushe Tawhiyd. Ni lazima kwa walinganizi waifanye Tawhiyd ndio kipaumbele katika maongezi yao yote; yawe machache au mengi. Wasipuuze Tawhiyd kwenye ndimi zao kwa hali yoyote. Kule kutoitilia kwake umuhimu kunaweza kuwafanya baadhi ya watu wakaona si lolote si chochote, jambo ambalo ni makosa. Bali inatakiwa, bali inasisitizwa kwa walinganiaji waanze na Tawhiyd katika hali zao zote.

Allaah amrehemu na kumsamehe Shaykh wetu ´Abdul-´Aziyz bin Baaz nimemsikia katika muhadhara wake akifanya Tawhiyd ndio ufunguzi wa ulinganizi wake. Sehemu kubwa ya maongezi yake, vitabu vyake na mihadhara yake ametoa kuhusu Tawhiyd. Kitabu chake “al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa”[1] ni muhadhara wenye thamani takriban kurasa 100 ambao aliutoa katika kilabu ya fasihi huko Makkah nadhani ilikuwa mwaka wa 405. Baada ya hapo ikawa ni kitabu chenye hadhi na thamani. Muhadhara huo ni kuhusu Tawhiyd na akaifanyia muhadhara maalum. Bali vitabu vyake (Rahimahu Allaah) ambavyo tumesikia na kuvisoma vyote vinatilia umuhimu suala la Tawhiyd hali ya kuilingania, kuifunza na kuisomesha. Huu ndio mwenendo wa wanazuoni, watu wenye ubora na maimamu wa ulinganizi (Rahimahumu Allaah) ambapo wanaitilia umuhimu na mkazo somo la Tawhiyd. Pindi tunapoona kundi lolote katika ndugu zetu wanazembea kuhusu Tawhiyd basi tunatakiwa kuwanasihi, kusaidiana nao, kuwaelekeza na kuwabainishia kuwa kutilia mkazo Tawhiyd hii ni miongoni mwa mambo matukufu zaidi.

[1] Tazama al-´Aqiydah as-Swahiyhah – Ibn Baaz – al-Firqah an-Naajiyah (firqatunnajia.com)

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalish-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.mufti.af.org.sa/ar/content/عدم-اهتمام-بعض-الدعوات-بالتوحيد
  • Imechapishwa: 11/06/2022