Iogopeni siku ambayo nafsi haitoifaa nafsi nyingine kwa lolote

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

  يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا شَفَاعَةٌ وَلَا يُؤْخَذُ مِنْهَا عَدْلٌ وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ

“Enyi wana wa Israaiyl! Ikumbukeni neema Yangu niliyokuneemesheni na hakika Mimi nimekufadhilisheni juu ya walimwengu wengineo. Na iogopeni Siku ambayo nafsi haitoifaa nafsi nyingine kwa lolote na wala haitokubaliwa kutoka kwake uombezi wowote na wala hakitochukuliwa kutoka kwake kikomboleo na wala hawatonusuriwa.”[1]

Kisha akawakariria wana wa israaiyl kuwakumbusha neema Yake hali ya kuwawaidhi, kuwatahadharisha na kuwahimiza na kuigopa siku ya Qiyaamah ambapo nafsi haitoifaa nafsi nyingine lolote. Haijalishi kitu hata kama nafsi inayotaka kunufaisha ni miongoni mwa nafsi zilizo tukufu kama mfano wa Mitume na waja wema. Aidha haijalishi kitu hata kama nafsi inayotaka kunufaishwa ni miongoni mwa nafsi za watu waliokaribu kiukoo. Nafsi haitonufaisha nyingine lolote kubwa wala dogo. Si vyenginevyo kitachomnufaisha mtu ni yale matendo yake aliyoyatanguliza.

وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا شَفَاعَةٌ

“… na wala haitokubaliwa kutoka kwake uombezi wowote.”

Bi maana nafsi yoyote ile haitokubaliwa kumwombea yeyote pasi na idhini ya Allaah na baada ya kumridhia yule mwenye kuombewa. Hakuna matendo yanayoridhiwa isipokuwa yale ambayo yamefanywa kwa ajili ya kutafuta uso wa Allaah na pia yawe yameafikiana na Sunnah.

وَلَا يُؤْخَذُ مِنْهَا عَدْلٌ

“… na wala hakitochukuliwa kutoka kwake kikomboleo.”

Allaah amesema:

وَلَوْ أَنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ مِن سُوءِ الْعَذَابِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ

“Lau wale waliodhulumu wangelikuwa na vile vyote vilivyomo ardhini na pamoja navyo mfano wake, basi bila shaka wangelifidia kwayo kutokamana na adhabu mbaya ya siku ya Qiyaamah.”[2]

Hilo halitokubaliwa kutoka kwao.

وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ

“… na wala hawatonusuriwa.”

Bi maana kuzuiliwa na yale mambo yenye kuchukiza. Kwa hivyo kumekataliwa kunufaika kutoka kwa viumbe kwa njia yoyote ile.

[1] 02:47-48

[2] 39:47

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 42
  • Imechapishwa: 16/07/2020