Inajuzu kwenda kwa kuhani, mpiga ramli na wachawi na kuwauliza na kujitibisha kwao kwa kutumia zaituni?

Swali 04: Inajuzu kwenda kwa kuhani, mpiga ramli na wachawi na kuwauliza na kujitibisha kwao kwa kutumia zaituni na mfano wake?

Jibu: Haijuzu kwenda kwa wapiga ramli, wachawi, wanajimu, makuhani na mfano wao. Wala haijuzu kuwauliza wala kuwasadikisha. Wala haijuzu kujitibisha kwao kwa kutumia zaituni wala kitu kingine. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuwaendea, kuwauliza na kuwasadikisha. Kwa sababu wanadai kujua mambo yaliyofichikana, wanawadanganya watu na wanaita katika sababu zinazopelekea kupotea kutokamana na ´Aqiydah. Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Yeyote atakayemwendea mpiga ramli na akamuuliza juu ya kitu, basi hazitokubaliwa swalah zake nyusiku arobaini.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayemwendea mpiga ramli au kuhani akamsadikisha kwa aliyoyasema, basi hakika ameyakufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Pia amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hatokamani na sisi yule mwenye kufanya uchawi au akaomba kufanyiwa uchawi, akafanya mkosi au akaomba kufanyiwa mkosi, akafanya ukuhani au akaomba kufanyiwa ukuhani.”

Zipo Hadiyth nyingi zilizokuja kwa maana kama hii.

Yale aliyohalalisha Allaah katika kujitibisha kwa kufanya matabano yanayokubalika Kishari´ah na madawa yaliyo halali kwa wale watu wanaotambulika kuwa na ´Aqiydah na historia nzuri ni yenye kutosheleza na himdi zote njema anastahiki  Allaah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Akhtwaau fiyl-´Aqiydah, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 07/08/2020