Inajuzu kwa msafiri kuswali nyumbani ilihali anasikia adhaana?

Swali 247: Je, inajuzu kwa msafiri kuswali katika nyumba alipofikia pasi na kwenda msikitini? Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah anapenda kuzitendea kazi ruhusa Zake.”

Jibu: Kuzitendea kazi ruhusa Zake ni kule kufupisha swalah. Ama kuswali katika mkusanyiko basi itambulike kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumpa idhini ya kuswali kwenye nyumba yake yule mwanaume kipofu. Alimwambia:

“Je, unasikia adhaana?” Akajibu: “Ndio.” Akamwambia: “Basi ni lazima uitikie.”

Jengine ni kwamba ipo Hadiyth ambayo kuna tofauti kuhusu kuitumia kama hoja, nayo ni ile inayosema:

“Mwenye kusikia wito na asiitikie basi hana swalah isipokuwa kutokamana na udhuru.”

Kinachonidhihirikia ni kwamba anapaswa kwenda msikitini na kuswali pamoja na waislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali Minaa msikitini wa al-Khayf na akaswali ´Arafah kwenye msikiti wa ´Arafah.

Kuhusu wanawake wakiwa nyumbani waswali mkusanyiko au waache kufanya hivo? Lakini bora ni wao kuswali mkusanyiko. Swalah ya mtu kwenye mkusanyiko inashinda swalah ya ambaye kaswali peke yake sokoni mwake au nyumbani kwake daraja ishirini na saba. Swalah ya kwenye mkusanyiko inashinda swalah ya aliyeswali peke yake kwa daraja ishirini na saba. Kwa hivyo wanawake waswali mkusanyiko.

Je, mwanamke [ambaye ni imamu] anatakiwa kusimama katikati yao au asogee mbele? Kinachonidhihirikia ni kwamba anatakiwa kusogea mbele na kwamba ni kama [imamu] mwanaume. Lakini wapo wanachuoni wenye kuona kwamba anatakiwa kusimama katikati yao.

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ijaabatu as-Saa-il, uk. 465
  • Imechapishwa: 31/10/2019