Imamu anapotoa salamu kabla sijamaliza Tashahhud

Swali: Ikiwa mswaliji amesahau ndani ya swalah yake, kisha imamu akatoa salamu hali yeye bado hajamaliza Tashahhud – Je, naye atoe salamu pamoja na imamu au achelewe ili akamilishe Tashahhud?

Jibu: Imamu akitoa salamu na wewe bado hujamaliza Tashahhud, basi unapaswa kuimaliza, kisha utoe salamu. Umalize kwanza Tashahhud na kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kisha utoe salamu. Ukimalizia pia kwa kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akukinge dhidi ya adhabu ya Jahannam, adhabu ya kaburi na maombi mengine yote yaliyokuja, basi hili ni bora. Baadhi ya wanazuoni wamesema du´aa hii ni wajibu. Kwa hiyo lililo bora ni kuikamilisha, kisha baada ya hapo utoe salamu. Unatakiwa usiwe mtu wa kughafilika, bali unatakiwa utunze usomaji wa Tahiyyaat ili uweze kutoa salamu mara moja pamoja na imamu. Jiepushe na kughafilika mpaka imamu atoe salamu na wewe bado upo katika kusahau. Inakupasa kujitahidi kukamilisha Tahiyyaat, kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuomba du´aa kabla imamu hajatoa salamu. Lakini tukikadiria kuwa imamu amemaliza na wewe hujamaliza, basi kamilisha, kisha utoe salamu.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1116/من-سها-حتى-سلم-الامام-ولم-يقرا-التشهد
  • Imechapishwa: 25/01/2026