´Abdullaah bin al-Mubaarak bin Waadhwih. Ni Imaam, Shaykh-ul-Islaam, mwanachuoni wa zama zake na kiongozi wa wachaji wa zama zake. Ni Abu ´Abdir-Rahmaan al-Handhwaliy al-Marwaziy. Alikuwa Haafidhw, mpambanaji na mmoja katika watu maarufu. Mama yake alikuwa kutoka katika kabila la Khuwaarizm.

Alizaliwa mwaka 118 na alianza kutafuta elimu wakati alipokuwa na miaka 20.

Katika waalimu wake wa kale kabisa ni ar-Rabiy´ bin Anas al-Khuraasaaniy. Alijipenyeza na akaingia kwake gerezani na akasikia karibu Hadiyth 40. Kisha akachukua kutoka kwa Taabi´uun waliokuwa wamebaki. Alifanya safari nyingi kwa ajili ya kutafuta elimu, kupigana vita, kufanya biashara, kuwasaidia ndugu zake kiuchumi na kuwapa ruzuku ili waweze kwenda kuhiji mpaka alipofariki.

Alisikia kutoka kwa Sulaymaan at-Taymiy, ´Aaswim al-Ahwal, Hishaam bin ´Urwah, al-A´mash, Yahyaa bin Sa´iyd al-Answaariy, Muusa bin ´Uqbah, al-Awzaa´iy, Abu Haniyfah, Ibn Jurayj, Ma´mar, ath-Thawriy, Ibn Abiy Dhi´b, Hammaad bin Zayd, Hammaad bin Salamah, Maalik, al-Layth, Ibn ´Uyaynah na wengineo.

Ma´mar, ath-Thawriy, Ibn Wahb, Ibn Mahdiy, Ibn Ma´iyn, Abu Daawuud, ´Abdur-Razzaaq bin Hammaam, al-Qattwaan na Hibbaan bin Muusa wamehadithia kutoka kwake.

Hadiyth yake ni hoja kwa maafikiano.

Ibn-ul-Mubaarak alisafiri Makkah, al-Madiynah, Shaam, Misri, ´Iraaq, Kurdistan na Khuraasaan na amehadithia kutoka maeneo mengi.

al-´Abbaas bin Musw´ab amesema:

“Mama yake na ´Abdullaah bin al-Mubaarak alikuwa anatokea Khuwaarizm na baba yake alikuwa anatokea Uturuki. Alikuwa ni mtumwa wa mfanyabiashara mmoja kutoka Hamadhaan.”

´Abdullaah bin al-Mubaarak amesema:

“Abu Haniyfah alimtazama baba yangu akasema: “Mama yake amemwacha kwako ikiwa ni amana.” Hakuna aliyekuwa anafanana sana na ´Abdullaah kama yeye.”

Nu´aym bin Hammaad amesema:

“Ibn-ul-Mubaarak alikuwa akiketi nyumbani kwa wingi. Akaambiwa: “Hivi huhisi upweke?” Akasema: “Ni vipi nitahisi upweke ilihali niko pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake?”

Ahmad bin Sinaan al-Qattwaan amesema:

”Nimefikiwa na khabari kwamba ´Abdullaah bin al-Mubaarak alimwendea Hammaad bin Zayd. Akamtazama, akapendezwa na hulka yake ambapo akasema: ”Unatokea wapi?” Akasema: ” Khuraasaan, kutokea Marw.” Akasema: ”Unamjua mtu anayeitwa ´Abdullaah bin al-Mubaarak?” Akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Yuko vipi?” Akasema: ”Ndiye huyu anayekuzungumzisha.”Akamsalimia na kumkaribisha.”

Ismaa´iyl al-Khuttwabiy amesema:

”Nimefikiwa na khabari kwamba Ibn-ul-Mubaarak alihudhuria kwa Hammaad bin Zayd, baadhi ya wanafunzi wakamwambia Hammaad: ”Muulize Abu ´Abdir-Rahmaan kama anaweza kutuhadithia [Hadiyth].” Akasema: ”Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Wameniomba nikwambie uwahadithie.” Akasema: ”Subhaan  Allaah! Ee Abu Ismaa´iyl! Nizugumze mbele yako?”Akasema: ”Nakuomba ufanye hivo.”Ndipo akasema: ”Abu Ismaa´iyl Hammaad bin Zayd ametuhadithia… ” na hakutaja herufi hata moja isipokuwa aliinasibisha kwa Hammaad.”

Ahmad al-´Ijliy amesema:

“Ibn-ul-Mubaarak alikuwa mwaminifu na imara katika Hadiyth. Alikuwa ni mtu mwema anayejua mashairi na alikuwa amekusanya elimu.”

Shu´ayb bin Harb amesema:

“Katu Ibn-ul-Mubaarak hakuwahi kukutana na mtu isipokuwa alikuwa ni bora kuliko yeye. Nimemsikia Abu Usaamah akisema: “Ibn-ul-Mubaarak katika Hadiyth ni kama Amiyr-ul-Mu´miniyn kati ya watu.”

Ismaa´iyl bin ´Ayyaash amesema:

“Hakuna juu ya uso wa ardhi mfano wa Ibn-ul-Mubaarak. Sioni sifa yoyote nzuri iliyoumbwa na Allaah isipokuwa itakuwepo kwa ´Abdullaah bin al-Mubaarak.”

Muhammad bin ´Aliy bin al-Hasan bin Shaqiyq ameeleza kuwa amemsikia baba yake akisema:

“Ulipokuwa unafika wakati wa hajj, basi Ibn-ul-Mubaarak alikuwa akiwakusanya marafiki zake kutoka Marw wakimzunguka na wakisema: “Tunafuatana nawe.” Anasema: “Nipeni pesa zenu.”Akichukua pesa zao, akiziweka ndani ya sanduku na akilifunga. Wakisafiri kutoka Marw kwenda Baghdaad na akiendelea kuwahudumia na akiwalisha chakula kizuri kabisa na vitu tamtam kabisa. Kisha akiwatoa kutoka Baghdaad kwenda katika mji wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakiwa katika mavazi mazuri kabisa. Halafu anamwambia kila mmoja: “Ni kipi familia yako wamekwambia uwanunulie kutoka al-Madiynah?” Kila mmoja anaanza kutaja kimoja baada ya kingine na anawanunulia. Kisha anawapeleka Makkah na baada ya kumaliza hijjah yao, anawaambia: “Ni kipi familia yako wamekwambia uwanunulie kutoka Makkah?” Kila mmoja anaanza kutaja kimoja baada ya kingine na anawanunulia. Halafu anawatoa Makkah kurudi Marw na huku akiendelea kuwagharamikia. Baada ya siku tatu anawafanyia sherehe na kuwavisha. Wakishakula na kufurahika, anaamrisha sanduku lile liletwe. Analifungua na anampa kila mmoja mkoba wake ukiwa na majina yao.”

Ibn Mahdiy amesema:

“Maimamu ni wanne: Sufyaan, Maalik, Hammaad bin Zayd na Ibn-ul-Mubaarak.”

Ibn Mahdiy amesema tena:

”Sijaona mjuzi zaidi wa Hadiyth kama Sufyaan, mwenye akili zaidi kama Maalik, mwenye kuipa nyongo dunia kama Shu´bah na mwenye kuutakia kheri zaidi Ummah kama Ibn-ul-Mubaarak.”

Ibn Mahdiy amesema:

” Ibn-ul-Mubaarak ni mjuzi zaidi kuliko Sufyaan ath-Thawriy.”

´Abdul-Wahhaab bin ´Abdil-Hakam amesema:

“Wakati Ibn-ul-Mubaarak alipofariki, kiongozi wa waumini Haaruun alisema: “Amekufa bwana wa wanachuoni.”

Abu Ishaaq al-Fazaariy amesema:

“Ibn-ul-Mubaarak ni Imaam wa waislamu wote.”

Nasema: “Imamu wa watu wa kipindi chake.”

´Aliy al-Madiyniy amesema:

“Elimu imekomeka kwa wanamme wawili; Ibn-ul-Mubaarak na Ibn Ma´iyn.”

Abu Wahb amesema:

“Ibn-ul-Mubaarak alipita karibu na bwana mmoja kipofu akamwambia: ”Nakuomba uniombee kwa Allaah anirudishie macho yangu.” Ndipo akamuomba Allaah amrudishie macho yake na mimi huku naona.”

al-Hasan bin ´Arafah amesema: “Ibn-ul-Mubaarak alinambia:

”Niliazima kalamu Shaam. Nilipofika Marw ndipo nikagundua kuwa bado niko nayo. Nikarejea Shaam na kurudisha kalamu kwa mwenye nayo.”

Aswad bin Saalim amesema:

”Ibn-ul-Mubaarak alikuwa Imaam anayechukuliwa kama mfano. Alikuwa ni miongoni mwa watu walio imara zaidi katika Sunnah. Ukimuona mtu anayemzungumza vibaya Ibn-ul-Mubaarak, basi utie ila Uislamu wake.”

Shu´bah amesema.

”Hatujawahi kufikiwa na yeyote kama mfano wa Ibn-ul-Mubaarak.”

Abu Usaamah amesema:

”Sijawahi kuona mtu anayetafuta elimu kama Ibn-ul-Mubaarak.”

”Kikosi cha al-Fadhwl bin Muusa na Makhlad bin al-Hasan kilikusanyika na kusema: ”Hebu tuhesabu sifa nzuri za Ibn-ul-Mubaarak; elimu, uelewa, adabu, sarufi, lugha, kuipa nyonyo dunia, ufaswaha, mashairi, kusimama usiku, ´ibaadah, hajj, kupigana vita, ushujaa, upandaji wanyama, nguvu, alikuwa hazungumzi juu ya mambo yasiyomuhusu, inswafu na uchache wa kutofautiana na marafiki zake.”

Habiyb al-Jallaab amesema:

”Nilimuuliza Ibn-ul-Mubaarak ni kitu gani bora alichopewa mtu?” Akasema: ”Ufahamu wa kina.” Nikasema: ”Asipokuwa nayo?” Akasema: ”Adabu nzuri.” Nikasema: ”Asipokuwa nayo?” Akasema: ”Ndugu anayemwelekeza.” Nikasema: ”Asipokuwa naye?” Akasema: ”Kunyamaza kwa muda mrefu.” ”Asipokuwa nayo?” Akasema: ”Kufa haraka.”

Inasemekana kwamba wakati Ibn-ul-Mubaarak alipofariki ar-Raashiyd alisema:

”Leo bwana wa wanachuoni amefariki.”

al-Hasan bin ar-Rabiy´ amesema:

“Punde tu kabla ya Ibn-ul-Mubaarak kufa alinambia: ”Nina miaka 63.”

al-Hasan bin ar-Rabiy´ amesema:

”Nilishuhudia kifo cha Ibn-ul-Mubaarak. Alikufa baada ya siku kumi Ramadhaan mwaka 181. Alifariki kipindi alipokuwa macho usiku na tukamzika Hiyt.”

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (8/378)
  • Imechapishwa: 08/10/2020