1- Baadhi ya watu wasiokuwa na elimu wanafikiria kimakosa kwamba ambaye amenuia kuchinja katika ´Iyd-ul-Adhwhaa kisha ndani ya masiku haya kumi akakata chochote katika nywele, kucha au ngozi yake, basi kichinjwa chake hakikubaliwi. Hili ni kosa la wazi. Hakuna mafungamano yoyote kati ya kukubaliwa kwa kichinjwa cha Udhhiyah na kukata hivyo vilivyotajwa hapo juu. Lakini ambaye atakata pasi na udhuru basi amekwenda kinyume na amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kujizuia na ametumbukia katika jambo lililokataza. Hivyo basi ni lazima kwake kumuomba Allaah msamaha na atubu Kwake na asirudi tena. Kuhusu kichinjwa chake cha Udhhiyah hakuna kizuizi cha kukubaliwa kwa sababu ya ukataji wake.

2- Ambaye atahitajia kukata nywele, kucha au chochote katika ngozi yake ambapo akafanya hivo, basi hakuna ubaya kwake. Kwa mfano amepata jeraha na hivyo akahitajia kukata nywele au kukata kucha zake kwa sababu zinamkera na hivyo akapunguza kutegemea na kile kiasi kinachomkera au ganda la ngozi yake inalea juujuu na kinamkera na hivyo akakikata, hakuna ubaya kufanya hivo.

3- Makatazo ya kukata nywele, kucha na chochote katika ngozi yake kwa atakayechinja yanakusanya mtu akinuia kujichinjia mwenyewe au kuitoa swadaqah kwa wegine.

Hapana shaka yoyote kwamba makatazo hayamuhusu mtu ambaye anachinja kwa niaba ya mtu mwengine.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (25/161)
  • Imechapishwa: 26/07/2020