Ibn ´Uthaymiyn na matembezi kwa ajili ya tanzia

1397-09-30

Kutoka kwa Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn kwenda kwa nduguye mtukufu …

السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

Jana nilipowapigia simu ili kuwapa pole juu ya kuondokewa na ndugu yenu (Rahimahu Allaah), ilinibainikia kuwa mmechukulia vibaya kwa sababu ya kutohudhuria nyumbani kwenu. Hili linaonyesha kuwa mimi nina nafasi ndani ya nafsi zenu, vinginevyo msingeona vibaya. Hata hivyo Allaah anajua kuwa sikuacha kuhudhuria nyumbani kwenu kwa ajili ya kuwadharau au kumchukulia si lolote wala chochote yule aliyepatwa na msiba. Lakini niliacha kufanya hivo kwa sababu haikuwa miongoni mwa mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Salaf watu kukusanyika kwa lengo la tanzia. Wakeze wawili wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walifariki kipindi cha uhai wake, ambapo mmoja ni Khadiyjah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ni wa kipekee na mama watoto wake wengi, pia walifariki watoto wake wote kipindi cha uhai wake isipokuwa tu Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa) na akasema kwa mnasaba wa kuondokewa na mtoto wake wa kiume Ibraahiym:

“Macho yanatokwa na machozi na moyo unahuzunika na hatusemi isipokuwa yale yanayomridhisha Mola wetu. Hakika ni wenye huzuni kwa kufarikina nawe, ee Ibraahiym.”[1]

Haikupokelewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alipanga mikutano ya tanzia baada ya kuondokewa na watu hawa. Kukaa kwake msikitini baada ya kufikiwa na khabari ya kufariki kwa Zayd, Ja´far na ´Abdullaah bin Rawaahah haina maana kwamba alikaa huko kwa lengo la tanzia.

Kutokana na kwamba kukusanyika pahali kwa lengo la tanzia haikuwa miongoni mwa mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Salaf, ndio maana lilimchukiza Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) tendo hilo na mara akasema kuwa haitakikani kufanya hivo na wakati mwingine akasema kuwa halimpendezi. Ibn Muflih amebainisha katika “al-Furuu´” kwamba pindi Imaam Ahmad anaposema kuwa haitakikani kufanya kitu fulani, basi anachomaanisha ni kwamba ni haramu kukifanya. Kwa ajili hiyo yamepokelewa makatazo na majuzisho kutoka kwake juu ya jambo hilo ambapo baadaye wafuasi wake waliokuja nyuma wamethibitisha kwamba kitendo hicho ni chenye kuchukiza. Ibn Muflih amesema katika “al-Furuu´”:

“Vikao kama hivyo vimechukizwa, kama alivosema. Maoni hayo yamechaguliwa na wengi, hali ya kuafikiana na Maalik na ash-Shaafi´iy.”

Katika “al-Muntahaa” na “al-Iqnaa”, ambavyo ndivo vyanzo vilivyokuja nyuma ya madhehebu, imekuja:

“Vikao kama hivyo vimechukizwa.”

Imekuja katika maelezo:

“Bi maana kwa ajili ya tanzia ambapo yule aliyefikwa na msiba huketi pahali fulani ili apewe pole au akaketi yule mwenye kutoa pole kwa aliyefikwa na msiba baada yake.”

Katika “al-Muhadhdhab”, ambacho ni moja katika vitabu vikubwa vya ash-Shaafi´iy kicheo, imekuja:

“Inachukiza kukaa pahali kwa ajili ya tanzia, kwa sababu kitendo hicho ni kitu kilichozuliwa na kitu kilichozuliwa ni Bid´ah.”

Katika maelezo imekuja:

“Maana yake ni kwamba wanakusanyika wale wanafamilia wa maiti katika nyumba fulani ili waje kupewa pole na watu. Badala yake wanatakiwa kuendelea na kazi zao za kila siku. Yule ambaye atakutana nao atawapa pole.”

Haya maneno niliyokutajieni ndio yaliyonifanya mimi kutokuja nyumbani kwenu kuwapa pole. Haihusiani na kuwadharau wala kumchukulia yule aliyefikwa na msiba si lolote si chochote. Bali mnayo kwangu ile heshima stahiki. Juzi nilikuwa na nafasi ya kuweza kuzungumza nanyi baada ya Fajr, lakini hata hivyo nisikitika kuwa haikuwezekana.

Kuhusu maiti, tunamuombea msamaha na rehema. Haya ndio niliyopenda kukubainishieni ili mweze kunifahamu. Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake na watakaomfuata mpaka siku ya Malipo.

[1] al-Bukhaariy (1303) na Muslim (2315).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/403-405)
  • Imechapishwa: 17/05/2021