Ibn Muflin kuhusu hukumu ya kuchinja katika ´Iyd-ul-Adhwhaa

Jopo la wanachuoni wengi wanaona kuwa kuchinja katika ´Iyd-ul-Adhwhaa imependekezwa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya hivo na akahimiza kitendo hicho na Ibn ´Abbaas ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimeamrishwa mambo matatu na yamependekezwa juu yenu; Witr, kuchinja na Rak´ah mbili kabla ya Fajr.”

Ameipokea ad-Daaraqutwniy.

Ahmad anayo maoni mengine yanayosema kuwa ni wajibu. Haya pia ndio maoni ya Abu Bakr [´Abdul-´Aziyz]. Hayo ni kutokana na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye nafasi na asichinje basi asisogelee uwanja wetu wa kuswalia.”[1]

Anayo maoni ya tatu yanayosema kuwa si wajibu isipokuwa kwa yule ambaye si msafiri.

Yuko na maoni mengine yanayosema kwamba ikiwa mtu yuko mwenye wepesi anatakiwa kuchinja. Hapa ndipo Abul-Khattwaab akaelewa kuwa ni lazima. Lakini hata hivyo mambo sivyo. Kwa sababu suala linahusiana na wepesi, na si kwamba kitendo hicho ni lazima.

[1] Ahmad (1/321), Ibn Maajah (3123), ad-Daaraqutwniy (2/545) na al-Haakim (4/231).

  • Mhusika: Imaam Ibraahiym bin Muhammad al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mubdi´ (3/297)
  • Imechapishwa: 11/07/2020