´Ibaadah anazofanya mwenye nifasi kabla ya siku arobaini

Swali: Je, inafaa kwa mwanamke mwenye damu ya uzazi kufunga, kuswali na kuhiji akitwahirika kabla ya siku arobaini?

Jibu: Ndio, inafaa kwake kufunga, kuswali, kuhiji, kufanya ´Umrah na ni halali kwa mumewe kumjamii akitwahirika ndani ya siku arobaini. Akitwahirika kwa muda wa siku ishirini basi atajisafisha, ataswali, atafunga na ni halali kwa mume wake.

Kuhusu yale yaliyopokelewa kutoka kwa ´Uthmaan bin al-´Aasw kwamba alichukizwa na jambo hilo yanafasiriwa kwamba ni machukizo ya kujitakasa. Aidha ni ijtihaad kutoka kwake (Rahimahu Allaah na Radhiya Allaahu ´ann). Ni kitu hakina dalili. Maoni ya sawa ni kwamba hapana vibaya kufanya hivo akitwahirika kabla ya siku arobaini. Damu ikimrejelea ndani ya siku arobaini maoni ya sahihi ni kwamba aizingatie kuwa ni damu ya uzazi midhali ni ndani ya muda siku arobaini. Lakini swawm, swalah na hajj yake ndani ya ule muda wa siku arobaini vyote ni sahihi. Hatorudia chochote katika hayo muda wa kuwa yametokea ndani ya utwahirikaji wake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/211)
  • Imechapishwa: 05/09/2021