Huyu ndiye mcheleweshaji anayepaswa kufunga na kulisha chakula

Swali: Ikiwa mtu amekosa siku kadhaa za Ramadhaan kwa sababu ya ugonjwa na ugonjwa huo ukaendelea mpaka Ramadhaan inayofuata, kisha baada ya hapo anatakiwa kulipa pamoja na kulisha chakula. Je, atoe kila siku peke yake au anaweza kutoa zote kwa pamoja kwa siku moja? Apewe nani? Je, pesa zinatosha?

Jibu: Ikiwa ugonjwa umeendelea kutoka Ramadhaan hadi Ramadhaan nyingine, basi hana wajibu wa kulisha chakula. Atalipa tu swawm tu, kwani ana udhuru. Ikiwa ugonjwa uliendelea naye hadi Ramadhaan nyingine, kisha Allaah akamponya baada ya Ramadhaan ya pili, basi atalipa siku alizokosa za Ramadhaan ya kwanza bila ya kulisha. Kulisha kunakuwa juu ya yule aliyepuuza na hakulipa mpaka Ramadhaan nyingine ikaingia bila ya udhuru. Huyu ndiye anayewajibika kulipa pamoja na kulisha, kama walivyofutu baadhi ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Anafunga siku alizoacha na analisha chakula kwa uzembe wake. Kwa kila siku atatoa nusu pishi ya chakula kinacholiwa katika mji. Hatoi pesa, bali anatoa chakula kama walivyotoa fatwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Anaweza kukusanya na kuwapa masikini kabla ya kufunga au baada ya kufunga.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3281/تاخير-قضاء-رمضان-الى-رمضان-الثاني-بسبب-المرض
  • Imechapishwa: 07/08/2026